Home BUSINESS BRELA YAKUTANA NA WADAU KUPITIA KANUNI ZA WAMILIKI MANUFAA

BRELA YAKUTANA NA WADAU KUPITIA KANUNI ZA WAMILIKI MANUFAA

Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), imekutana na Vyombo vya Uchunguzi kupitia Kanuni za Wamiliki Manufaa wa Kampuni zinazomilikiwa na Wabia kwa lengo la kuziboresha.

Akifungua warsha ya siku moja katika ukumbi wa Zimamoto, Jijini Dodoma, mapema leo tarehe 02 Machi, 2023, kwa niaba ya Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA Bw. Godfrey Nyaisa, Kaimu Mkurugenzi wa Makampuni na Majina ya Biashara Bw. Meinrad Rweyemamu amesema lengo la warsha hiyo ni kupeana elimu ya kiutendaji kwa wadau na watumiaji wa taarifa za Wamiliki Manufaa.

“Kama ilivyokuwa ada BRELA tumekuwa tukishirikiana na wadau kwenye shughuli zetu mbalimbali za kiutendaji ikiwa ni pamoja na kufanya maboresho mbalimbali ya kisheria na kimfumo lengo ni kuhakikisha BRELA inatoa huduma bora kwenu na kwa umma kwa ujumla”, amefafanua Bw. Rweyemamu.

Bw. Rweyemamu amesema kuwa Kampuni zina umuhimu mkubwa katika kuchangia uchumi wa nchi, hata hivyo uzoefu umeonyesha kwamba kampuni nyingine zinatumika vibaya katika kufanya vitendo vya uhalifu ikiwa ni pamoja na utakatishaji wa fedha haramu, kufadhili vitendo vya ugaidi, vitendo vya rushwa na hata ukwepaji wa kodi.

Kutokana na hali hiyo amesema Benki ya Dunia na taasisi nyingine za Kimataifa zinazojihusisha na masuala ya kusaidia biashara zimejitolea kwa njia moja au nyingine kuleta mabadiliko kwa kuanzisha dhana ya Wamiliki Manufaa ( Beneficial Ownership concept) ambayo imeungwa mkono na Jumuiya ya Kimataifa.

Ameongeza kuwa Tanzania ni moja ya nchi ambazo zipo chini ya Eastern and Southern Anti-Money Laundering Group ( ESAMLAG), ambapo lengo kuu la ESAMLAG ni kuhakikisha kuwa mapendekezo 40 ya Financial Action Task Force yanafanyiwa kazi na moja kati ya mapendekezo hayo ni kuhakikisha nchi inaanzisha daftari la Wamiliki Manufaa wa Kampuni na kuhakikisha vyombo vya Uchunguzi vinapata taarifa za Wamiliki Manufaa kwa wakati.

Aidha ameongeza kuwa Sheria ya Kampuni Sura 212 ilifanyiwa marekebisho kupitia Sheria ya Fedha, 2020 kwa kuleta dhana ya Umiliki Manufaa wa Kampuni. Marekebisho haya yalienda sambamba na utungwaji wa Kanuni za Wamiliki Manufaa za mwaka 2021 ambazo zinatumika katika kusimamia zoezi la ukusanyaji, uwasilishaji na utoaji wa taarifa za wamiliki manufaa wa kampuni.

Amesema pia Wakala imeona ni vyema kuandaa warsha hii ya kuwashirikisha wadau mbalimbali kujadili na kukusanya maoni yao ili kuboresha rasimu ya Kanuni zilizoandaliwa na kuweka utaratibu madhubuti utakaowezesha upatikanaji wa taarifa za wamiliki manufaa wa Majina ya Biashara pamoja na utoaji wa taarifa hizo kwa vyombo vya upelelezi vilivyoainishwa kwenye Sheria pale zinapohitajika.

Aidha, Bw. Rweyemamu amewashukuru wadau kwa ushirikiano mzuri na kuwaahidi kuboresha huduma kwa njia ya mtandao na kushughulikia changamoto mbalimbali pamoja na kupokea maoni yatakayopelekea kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma kwa wananchi.

Previous articleMAKAMU WA RAIS ATEMBELEA KITUO CHA HUDUMA ZA PAMOJA CHA AZERBAIJAN
Next articleDC MAGEMBE, AJA NA MKAKATI MPYA KUDHIBITI MATUKIO YA MAUAJ WILAYA YA GEITA.
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here