Baadhi ya watumishi na wadau wa mahakama mkoani Ruvuma wakiwa katika maandamano kabla ya kufungwa kwa wiki ya sheria nchini,ambayo kimkoa imefanyika katika viwanja vya mahakama kuu kanda ya Songea.
Jaji mfawidhi wa mahakama kuu kanda ya Songea Dkt Yose Mlyambina akikagua gwaride la heshima mara baada ya kuzungumza na wananchi,watumishi na wadau wa mahakama kwenye kilele cha maadhimisho ya wiki ya mahakama iliyofanyika katika viwanja vya mahakama kuu mjini Songea,
Jaji Mfawidhi wa Mahakama kuu kanda ya Songea Dkt Yose Mlyambina katikati,Jaji wa mahakama kuu kanda ya Songea Mheshimiwa Upendo Madeha wa pili kushoto,Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Kanal Laban Thomas wa pili kulia,Mkuu wa Brigedi ya 401 Songea Brigedia Jenerali Charles Feruz wa kwanza kushoto na Mkuu wa wilaya ya Songea Wilman Ndile kulia,wakiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama mkoa wa Ruvuma.
Watumishi wa mahakama wakiimba wimbo maalum wa maadhimisho ya wiki ya sheria katika viwanja vya mahakama kuu mjini Songea.
Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Kanal Laban Thomas akizungumza na wananchi na wadau wa sheria kwenye kilele cha wiki ya sheria ambayo kimkoa imefanyika katika viwanja vya mahakama kuu mjini Songea.
Jaji mfawidhi wa mahakama kuu kanda ya Songea Mheshimiwa Dkt Yose Mlyambina akimpa cheti maalum mkuu wa Magereza(RPO) mkoa wa Ruvuma Willington Kahumuza kutokana na mchango wa Jeshi hilo kutoa elimu ya sheria kwa wananchi katika maadhimisho ya wiki ya sheria,
Na: Muhidin Amri, Songea
ZAIDI ya wakazi 7,200 wamefikiwa na elimu ya sheria na namna ya kumaliza migogoro kwa njia ya usuluhishi katika muda wa wiki moja ya maadhimisho ya sheria yaliyoanza tarehe 22 hadi tarehe 29 Januari mwaka huu wilyani Songea.
Hayo yamesemwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama kuu kanda ya Songea Dkt Yose Mlyambina, wakati akifunga maadhimisho ya wiki ya sheria ambayo kanda ya Songea yamefanyika katika viwanja vya Mahakama kuu wilayani Songea.
Jaji Mlyambina,amewataka wadau utoaji haki kuongeza juhudi katika kutatua changamoto mbalimbali ikiwamo mashauri na migogoro ya ardhi ili jamii iweze kupata haki kwa wakati.
Alisema,migogoro na mashauri yakimalizwa ipasavyo itawezesha kuharakisha maendeleo ya mtu mmoja mmoja na kuharakisha uchumi wa nchi kwa kuwa jamii itapata nafasi kubwa ya kujikita kwenye shughuli za uzalishaji mali.
Kwa mujibu wa Jaji Mlyambina,usuluhishi ni moja ya njia sahihi na nzuri za kutatua migogoro mbalimbali katika jamii na kuomba wadau wa mahakama kuongeza nguvu na kuharakisha utatuzi wa mashauri yanayofikishwa katika maeneo yao kwa njia hiyo.
Aidha amewataka wadau hao kujikita zaidi katika mfumo wa utoaji haki kuendelea kutoa elimu kwa umma na kuhakikisha huduma mbadala ya usuluhishi inapatikana na kufikiwa kwa urahisi na kuimarisha utatuzi ili kufikia malengo.
Katika hatua nyingine Jaji Mlyambina amewaasa mawakili wa kujitegemea kujielekeza katika kutoa elimu na ushauri sahihi kwa wateja wao kuhusu namna bora ya kutatua migogoro ikiwa ni pamoja na kutumia njia mbadala ya usuluhisi badala ya kuendelea na kesi mahakamani ambako watalipwa gharama kubwa zaidi za kutetea wateja wao.
Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Thomas Laban amempongeza Jaji mfawidhi wa Mahakama kuu kanda ya Songea Dkt Yose Mlyambina kwa kwa kusimamia vizuri suala ya utoaji haki kwa wananchi wanaofika mahakamani kwa ajili ya kutafuta na kudai haki zao za msingi.
Laban alisema,tangu alipofika mkoani Ruvuma kama Mkuu wa mkoa na mwenyekiti wa kamati ya maadili kwa Mahakimu hajapokea malalamiko yoyote kutoka kwa wananchi wakilalamikia kunyimwa haki na mahakimu au wadau wengine wa sheria.
Alisema,utatuzi wa migogoro iliyopo katika jamii ni haki ya msimgi ya kila mtu ambapo amewataka mahakimu na watumishi wengine wanaofanya kazi katika vyombo vya kusimamia na kutoa haki kuongeza nguvu na kutatua migogoro kwa njia ya usuluhishi na haki badala ya kutatua migogoro kwa upendeleo.
Mkuu wa mkoa,ameliomba Jeshi la Polisi kama wadau wakubwa wa Mahakama nchini,kuanza kutatua migogoro kwa njia ya kusuluhisha migogoro inayofikishwa kwenye vituo vya polisi na kutosita kutoa ushauri kwa wananchi kumaliza tofauti (migogoro) yao kwa njia ya amani badala ya kufikishana mahakamani.
Aidha,amewaagiza wenyeviti wa mabaraza ya ardhi na nyumba kuongeza kasi ya kusikiliza mashauri ili wananchi wapate muda wa kuendelea kufanya kazi nyingine za uzalishaji mali na siyo kutumia muda wao mwingi kwenda kusikiliza mashauri.
Katibu wa Baraza kuu la Waislamu(Bakwata)mkoani Ruvuma Rajabu Songambele,amewataka watumishi wa mahakama k kutunza siri za serikali na kutenda haki kwa wananchi wengine ili kuepusha nchini kuingia kwenye migogoro inaweza kurudisha nyuma maendeleo ya nchi.
Alisema,watumishi na wasimamizi wa sheria nchini,ni vyema wakatenda haki kwa wananchi wanaofika katika maeneo yao ya kazi kudai na kutafuta haki zao, badala ya kupendelea upande usio kuwa na nguvu ya kifedha au madaraka.
Mwenyekiti wa Chama cha Wanasheria Tanganyika(TLS) mkoa wa Ruvuma Edson Mbogoro,ameipongeza Mahakama nchini kwa kufanya mabadiliko makubwa ya kiutendaji ambayo yanakwenda kuisaidia jamii kupata haki kwa wakati.