Na: WAF- Kilimanjaro.
Watu wanaoishi na ulemavu wameiomba Serikali kupitia Wizara ya Afya kuwasaidia kupunguza gharama za vifaa vyao vinavyowasaidia kutembea ikiwemo viti mwendo ili kila mwenye ulemavu aweze kuvipata kwa urahisi.
Ombi hilo limetolewa mkoani Kilimanjaro na mwakilishi na mnufaikaji wa huduma za taasisi ya CCBRT Bi Flora katika sherehe za maadhimisho ya miaka 25 ya taasisi ya CCBRT yaliyoongozwa na Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel na Wakuu wa Mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Tanga.
“Tunathamini mchango mkubwa uliofanywa na Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan katika kuwasaidia wenye ulemavu nchini, ikiwemi kutoa mikopo isiyo na riba, lakini tunaiomba sana Serikali kuangalia juu ya kupunguza gharama za vitimwendo ili mwenye ulemavu aweze kuvimudu.” Amesema Flora.
Sambamba na hilo wameiomba Serikali iwasaidie kupata huduma za Bima na kuingiza baadhi ya huduma za msingi kwenye huduma za Bima, ili kuondokana na tatizo la gharama kubwa za matibabu wanalokumbana nalo katika kipindi hiki.
Aidha, watu hao, wameiomba Serikali kuongeza kutoa kipaumbele cha ajira kwa watu wanaoishi na ulemavu, hali itayosaidia kupunguza utegemezi kwa ndugu ma jamaa katika jamii.
Wakati akifungua maadhimisho hayo, Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan tayari imetoa mikopo isiyo na riba kwa watu wenye ulemavu kupitia halmashauri ili kusaidia kuwakwamua katika uchumi na itaendelea kufanya hivyo.
Pamoja na hayo, ametoa wito kwa wananchi kujenga tabia ya kuwasaidia watu wenye uhitaji, ikiwemo wenye ulemavu kuliko kutoa fedha nyingi kwenye shughuli zisizo na faida katika jamii.
Kwa upande mwingine, amewaelekeza mfuko wa Bima ya Afya ya taifa kufanya maboresho kwenye mfuko huo kwa kuingiza huduma za watu wenye ulemavu ili waondokane na changamoto ya gharama kubwa za matibabu ya afya zao.
Mwisho.