Na: Farida Mangube, MOROGORO
Wathamini wa serikali na sekta binafsi kutoka mikoa mbalimbali hapa nchini wamekutana mkoani Morogoro kujifua kwa ajili ya kuangalia namna bora ya kuweza kujitetea mahakamani pamoja na kutatua changamoto za malalamiko ya wananchi, kutokana na kuwepo kwa baadhi ya wathamini kushindwa kujitetea mahakamani hivyo kupelekea kushindwa kuapata ushindi kwenye kesi.
Akizungumza mara baada ya mafunzo ya kuwajengea uwezo wathamini hao Mwenyekiti wa Bodi ya Wathamini nchini Dakta Cleutus Njovu amesema wamelazimika kufanya mafunzo hayo kwa wathamini nchini ili kuwasaidia wathamini kujiamini mahakamani na kutoa ushahidi wa kuaminika ili kuilinda taaluma yao.
Aidha Mwenyekiti wa Bodi ya Wathamini nchini Dakta Njovu amesema dhumuni kubwa la mafunzo hayo ni kuwasaidia wathamini kuondoa uoga wakishakuwa mbele ya Jaji ili kutoa utetezi uanostahili.
Kwa upande wake Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu ya Tanzania ambaye pia ni muwezeshaji wa mafunzo hayo Dakta Atuganile Ngwala amesema pamoja na wathamini hao kuwa na utaalamu lakini ni vyema kujikukumbusha mara kwa mara mambo ya kuzingatia kama sheria, kanuni na taratibu katika kazi zao ili kuhakikisha wanafanya kazi kwa ufanisi.
“Hata kama ungekuwa unajua lakini kuna umuhimu sana wa kujikumbusha na kujinoa kwa yale mambo ambayo pengine wakati mwingine wanakutana nayo na wakati mwingine wanakutana na changamoto mbalimbali wanapokuwa mahakamani “ Amesema Dakta Ngwala.
Nao wathamini kutoka mikoa mbalimbali wamesema kuwa mafunzo hayo yatawasaidia katika kuwaweka vizuri mthamini kuwa shahidi mzuri kwenye vyombo vya sheria kama mahakama, pale tu watakupoitwa kutoa ushahidi.
Aidha wamesema kuwa wathamini wana mchango mkubwa kwenye jamii, kwa kufanya kazi kuwafanyia uthamini wa mali zake pale tu endapo wanahitaji kuchukua mkopo kwenye benki au pale tu kupigwa mnada na benki, hali kadhalika kwenye mambo mengine ambayo yanahitaji mthamini.