Na: Hughes Dugilo, DAR ES SALAAM
WAFANYABIASHARA 250 kutoka Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) wamethibitisha kushiriki katika Kongamano la Kimataifa la Biashara kati ya nchi za Jumuiya ya Ulaya na Tanzania linalotarajiwa kufanyika kwa siku mbili kuanzia Februari 23 na 24, 2023 katika Ukumbi wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNlCC) Jijini Dar es Salaam..
Akizungumza leo Februari 17,2023 wakati wa mkutano wa Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Dkt. Ashatu Kijaji alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu Kongamano hilo ambapo TPSF na wadau wengine waliudhuria, Mtatuzi wa Changamoto za Kibiashara kutoka TPSF Kinanasy Seif amesema taasisi hiyo imejiandaa kikamilifu kushiriki kongamano hilo.
Ametumia nafasi hiyo kueleza kwamba wafanyabiashara watakaoshiriki wametoka sekta za kilimo, madini, viwanda,biashara pamoja na usafirishaji huku akifafanua TPSF inaamini kongamano hilo litaongeza wigo kwa wafanyabiashara kupata masoko katika soko la Ulaya kutokana na mikataba ya kibiashara itakayosainiwa wakati wa kongamano hilo.
“Baada ya kuingia ubia tunaamini milango itakuwa imefunguka kwa bidhaa za Tanzania kuanza kuuzwa kwenye soko la Ulaya, na hiyo itasaidia kukua kwa uchumi wetu kutokana na uzalishaji kuongezeka na soko la ajira litakua,”amesema.
Aidha ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji nchini na kuweka mazingira wezeshi ya ufanyaji Biashara hapa nchini.
TPSF ikiwa kama Injini ya uchumi inashiriki Kongamano hilo linalofanyika kwa mara ya kwanza nchini Tanzania kama mdau mkubwa wa Sekta Binafsi huku ikiwa na matumaini makubwa ya Kongamano hilo litaongeza fursa kwa wafanyabiashara wa Tanzania.