Naibu Gavana Utawala na Udhibiti wa ndani Benki kuu ya Tanzania (BoT) Bw. Julian banzi akizungumza alipokuwa akifungua kikao kati ya BoT na Wahariri wa vyombo vya habari uliofanyika leo Februari 27,2023 katika ukumbi wa Benki hiyo Jijini Dar es Salaam.
Meneja Msaidizi Idara ya Mawasiliano Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Noves Mosses akizungumza alipokuwa akitoa salamu za utangulizi akimkaribisha Naibu Gavana kufungua rasmi Mkutano huo.
Kaimu Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) Bw. Bakari Machumu akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa Jukwaa hilo Deodatus Balile katika Mkutano huo uliofanyika leo Februari27,2023Jijini DaresSalaam.
Afisa Uhusiano Mkuu wa BoT Lwaga Mwambande (wa kwanza kulia) akiwa na Baadhi ya wahariri wa habari katika mkutano huo.
Baadhi ya Wahariri wa habari waliohudhuria mkutano huo.
(PICHA NA HUGHES DUGILO)
Naibu Gavana Utawala na Udhibiti wa ndani Benki kuu ya Tanzania (BoT) Bw. Julian banzi (mwenye suti ya Bluu) akiwa katika picha ya pamoja na Wahariri wa vyombo vya habari pamoja na Maofisa wa Benki.
Na: Hughes Dugilo, DAR
Naibu Gavana wa Benki kuu ya Tanzania (BoT) Julian Banzi amewataka wahariri wa vyombo vya habari hapa nchini kutumia vyema kalamu zao ili kupeleka taarifa za kiuchumi na fedha kwa wanachi kwa lengo la kuchochea maendeleo katika jamii.
Naibu Gavana huyo ameyasema hayo leo Februari 27, 2023 wakati wa ufunguzi wa Mkutano Maalumu kati ya Benki hiyo na wahariri wa vyombo vya habari nchini uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa BoT Jijini Dar es salaam ambapo amesema mkutano huo utasaidia kuongeza uelewa wa elimu ya uchumi na fedha.
“Ni matumaini yangu kwa kupitia mkutano huu kutaongeza chanchu kwenu wahariri kuweza kuandika taarifa zinazohusu mambo ya uchumi na fedha vizuri zaidi ili wananchi na jamii kwa ujumla ipate taarifa za kuaminika juu ya shughuli mbalimbali zinazofanywa na Beki kuu ya Tanzania” amesema Bw. Banzi.
Aidha ameeleza kuwa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania liliipa dhamana Benki hiyo ya kusimamia Sekta ndogo za Fedha (Microfinance) zinazojihusisha kutoa mikopo kwa wananchi na kwamba mkutano huo utawapa nafasi wahariri kufahamu namna ambavyo BoT inavyoisimamia Sekta hiyo.
Amefafanua kuwa hapo awali kabla ya BoT kupewa jukumu hilo kulikuwa na changamoto kwa Taasisi zinazotoa huduma ndogo za fedha kwa kutoa mikopo umiza kwa wananchi na kujikuta wakijiingiza kwenye matatizo kwa kushindwa kumudu mikopo hiyo.
“Sekta hii imekuwa ikikimbiliwa na wananchi wengi na kujikuta wanaingia kwenye matatizo kutokana na ukiukwaji wa kanuni na sheria katika utoaji wa mikopo hiyo ambayo imekuwa ikiwaumiza wananchi, hivyo ni vizuri mkapata nafasi ya kuelezwa kuhusu sekta hiyo ndogo ya fedha na changamoto zilizokuwepo.” amefafanua Naibu Gavana Banzi.
Kwa upande wake Kaimu Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) Bakari Machumu amesema mkutano huo uliolenga kuwajengea uwezo wahariri wa vyombo vya habari pamoja na waandishi wa habari utawawezesha kupeleka taarifa zilizo sahihi juu ya mambo ya kiuchumi.
Amesema kuwa kwa sasa nchi inapita katika mapinduzi ya kiuchumi hivyo kama vyombo vya habari visipokuwa na uelewa juu ya masuala ya kiuchumi na fedha vinaweza kutoa taarifa ambazo sio sahihi juu ya mambo hayo.
Amewapongeza BoT kwa kutoa elimu hiyo na kutoa mwito kwa Benki hiyo kupita katika vyuo mbalimbali vya uandishi wa habari ili kutoa elimu kwa wanafunzi wanaosoma katika vyuo hivyo na hatimaye waje kuwa wanataaluma wenye uelewa katika kuandika habari za uchumi na fedha.