Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Selemani Jafo wakati akizungumza na waandishi wa habari leo Februari 03, 2023 jijini Dodoma katika mkutano uliohudhuriwa pia na baadhi ya viongozi kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais.
(PICHA NA OFISI YA MAKAMU WA RAIS)
Serikali imetoa siku saba kwa maeneo yote yanayofanya uchafuzi wa mazingira unaotokana na kelele na mitetemo kurekebisha changamoto hiyo na kulielekeza Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kuyafungia maeneo yatakayokaidi maelekezo hayo.
Pia imewataka wamiliki wa maeneo ya burudani, starehe na nyumba za ibada kuzingatia matumizi ya vipima kelele na vizuia sauti ili kuhakikisha jamii zinazozunguuka maeneo hayo haziathiriwa na kelele wanazozisababisha.
Hatua hiyo imekuja kutokana na kuongezeka kwa malalamiko ya kelele na mitetemo mwaka 2021/2022 ambapo asilimia 65 ya malalamiko yaliyowasilishwa NEMC yanahusu kelele na mitetemo, hali inayoonesha adhabu za kutozwa faini kwa wanaokamatwa zimezoeleka na hazitoshi.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Selemani Jafo wakati akizungumza na waandishi wa habari leo Februari 03, 2023 jijini Dodoma.
Amesema kwa mujibu wa Sheria ya Mazingira Sura ya 191, Kifungu cha 106 (5 na 6) kinakataza kupiga kelele kuzidi viwango vilivyoruhusiwa na vilevile ni kosa kupiga kelele kinyume na viwango vilivyoruhusiwa.
Hata hivyo uchafuzi wa mazingira unaosababishwa na kelele na mitetemo ni miongoni mwa kero kubwa inayohatarisha afya ambapo na Shirika la Afya Duniani (WHO) limebainisha kelele kuwa ni mojawapo ya vitu hatarishi katika maisha ya binadamu na kwa mujibu wa “European Environmental Agency” (EEA, 2018) kelele ni kisababishi cha vifo vya mapema kwa watoto “Pre-mature death”.
“Kanuni za udhibiti wa kelele na mitetemo za mwaka 2015, zimeainisha viwango vya sauti vinavyoruhusiwa kwenye maeneo ya makazi, biashara, viwanda na hospitali ili kulinda afya ya jamii hivyo, nitoe wito kwa wananchi kutoa taarifa kuhusu kelele na mitetemo kwenye ofisi za serikali za mitaa au ofisi za NEMC,” amesema.
Aidha, Dkt. Jafo amezitaka Wizara za kisekta, Taasisi za umma, Sekretarieti za mikoa, Mamlaka za serikali za mitaa kuhakikisha zinatekeleza majukumu yao yaliyoainishwa kwenye mwongozo wa udhibiti wa uchafuzi wa mazingira utokanao na kelele na mitetemo wa mwaka 2021.
Itakumbukwa Julai 29, 2019 Serikali ilielekeza kuwa wadau wote wanaohusika kuhakikisha wanazingatia sheria na miongozo inayodhibiti uchafuzi wa mazingira unaotokana na kelele na mitetemo na pia hatua kali za kisheria zichukuliwe kwa wale ambao shughuli zao zinasababisha kelele kuzidi viwango vilivyoainishwa.
Hatua za kisheria zilizoainishwa kwenye sheria ni pamoja na kutozwa faini na kufungiwa biashara kwenye maeneo yaliyokithiri kwa kelele na mitetemo.