Home BUSINESS SERIKALI KUIMARISHA SEKTA YA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI KUPITIA ASDP II

SERIKALI KUIMARISHA SEKTA YA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI KUPITIA ASDP II

Na:  Mwandishi Wetu

Serikali Kupitia Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili (ASDP II) inayoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu, imesema imedhamiria kuongeza tija ya uzalishaji kwa wakulima, wavuvi pamoja na wafugaji nchini ili kuwawezesha kupata faida katika shughuli zao za kujiongezea kipato katika sekta husika.

Akizungumza Jijini Dar es Salaam, katika Mkutano wa Makatibu Wakuu kutoka Wizara za kisekta pamoja na Wadau wa Maendeleo ya Kilimo, Uvuvi na Ufugaji Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, Dkt. John Jingu alisema kuwa Serikali inadhamiria kuwainua wakulima, wavuvi na wafugaji ili wazalishe kwa tija kubwa.

“Tumefanya Mkutano wa Makatibu Wakuu kutoka sekta husika na wadau wa maendeleo ya kilimo,uvuvi na ufugaji ili kutathmini ASDP II na kuhakikisha kuwa suala la kilimo linatekelezwa kwa tija na kuleta faida kwa wakulima wetu ili liweze kuchangia kwa kiwango kikubwa zaidi kuliko ilivyo sasa katika maendeleo ya nchi yetu”, Alisema Dkt. Jingu.

Aidha, Dkt. Jingu alisema kuwa kuna programu mbalimbali ambazo Serikali imeanzisha kwenye sekta ya kilimo, uvuvi na ufugaji zote zikiwa na lengo la kuwawezesha wakulima, wavuvi na wafugaji kufanya shughuli zenye tija ikiwemo kutumia teknolojia Madhubuti, kupata matokeo makubwa kwa kutumia rasilimali chache na kutumia mbinu za kisasa zaidi kwenye uzalishaji kwa maendeleo zaidi.

“Kuna jitihada ambazo zinafanywa na Wizara za kisekta ili kuwawezesha wanaojihusisha na shughuli za uzalishaji katika maeneo mbalimbali watumie rasilimali kidogo na kupata matokeo makubwa katika uzalishaji wa shughuli zao”, Alisema Dkt. Jingu.

Kwa Upande wake Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Nazael Madalla amesema kuwa Programu ya ASDP II imefanikisha mambo mengi katika sekta za uvuvi na ufugaji ambapo kwa sasa utekelezaji wake unaendelea kuwanufaisha wahusika wa shughuli hizo.

“Kupitia Programu ya ASDP II katika sekta ya uvuvi kuna ujenzi wa Bandari Kubwa ya uvuvi ambayo inajengwa Kilwa Masoko Wilayani Kilwa Mkaoani Lindi na itasaidia katika kuhudumia meli kubwa za uvuvi na kuwasaidia wavuvi kufanya kazi kwa tija”, Alisema Dkt. Madalla.

Aidha, Dkt. Madalla alisema kuwa Wizara ikishirikiana na Benki ya Maendeleo ya Kilimo nchini kwa mwaka huu wa fedha 2022/23 itaanza kutoa mikopo ya boti za uvuvi ambazo zitafanya wavuvi kufanya kazi kwa tija kubwa lakini pia Wizara itatoa mikopo kwa ajili ya ufugaji wa Samaki.

Naye, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Dkt. Maduhu Kazi amesema kuwa program hiyo ni muhimu kwani Taasisi za Wizara hiyo ikiwemo Jeshi la Magereza na Jeshi la Polisi kupitia mashirika yake ya uzalishaji ambayo yanajihusisha na kilimo, uvivi pamoja na ufugaji.

“Sisi Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi tumealikwa kwenye kikao hiki cha kutathmini Programu ya ASDP II kwa sababu sisi kama wizara tuna Taasisi zinazojihusisha na kilimo, uvuvi na ufugaji, tuna Jeshi la Magereza na Jeshi la Polisi ambapo mashirika yake yanafanya uzalishaji katika kilimo, uvuvi na ufugaji na yana mlengo wa kibiashara pamoja na uwekezaji”, Alisema Dkt. Maduhu.

Programu hiyo ilianza takribani miaka 20 iliyopita na kufanyika kwa mkutano huo ni kutathmini wapi sekta hizo zimetoka, zilipo na kuona namna gani zinaweza kwenda mbele zaidi katika uzalishaji ili ziweze kuchochea mandeleleo ya wakulima, wavuvi, wafugaji pamoja na mchango katika maendeleo ya nchi.

Mwisho

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here