Home LOCAL NAIBU WAZIRI MASANJA AITAJA MWANZA KUWA KITOVU CHA UTALII

NAIBU WAZIRI MASANJA AITAJA MWANZA KUWA KITOVU CHA UTALII

Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mwanza na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja amesema jiji la Mwanza linatarajiwa kuwa kitovu cha utalii kwa kuwa na ongezeko la uwekezaji katika Sekta ya Utalii na kuwa na ongezeko la mnyororo wa thamani wa mazao yatokanayo na utalii.

Ameyasema hayo Februari 4,2023 wakati wa Kumbukizi ya Miaka 46 ya Kuzaliwa kwa Chama cha Mapinduzi yaliyofanyika katika uwanja wa Furahisha jijini Mwanza.

“Ninatambua kwamba pamoja na miradi inayotekelezwa katika Mkoa wa Mwanza, Sekta ya Maliasili na Utalii haijasahaulika na Mkoa wa Mwanza umependekezwa kuwa kitovu cha utalii” Mhe. Masanja amesisitiza.

Amefafanua kuwa kutokana na miradi ya kimkakati inayotekelezwa chini ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan itapelekea Mwanza kufaidika na uwekezaji unaotokana na Sekta ya Utalii.

Amesema miradi ya ujenzi wa reli, stendi ya Nyegezi na Nyamhongolo, kiwanja cha ndege, Daraja la Magufuli la Kigongo-Busisi na miradi mingine itasaidia watalii kufika jijini Mwanza na hatimaye wananchi kufaidika na utalii.

“Tunatambua kuwa Rais Samia alizindua Royal Tour, hivyo kutokana na uwekezaji huo kila mwananchi anaguswa na mnyororo wa thamani unaotokana na utalii mfano mgeni anapokanyaga Mwanza wafanyabiashara wadogo watafaidika kama wauza machungwa, chakula na huduma za malazi” Mhe. Masanja amesema.

Ameweka bayana kuwa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ana mipango mikubwa na Mwanza na Mwanza itakuwa ni jiji namba moja linalotambua uwekezaji unaotokana na Sekta ya Utalii.

Aidha , Mhe Masanja amewahimiza wananchi kuwa na tabia ya kupanda miti ili kuifadhi mazingira na kutunza uwepo wa hali ya hewa nzuri kwa manufaa ya sasa na vizazi vijavyo.

Previous articleVIWANDA VYA NGUZO ZA MITI ZA UMEME KATIKA MIKOA YA MARA NA KIGOMA VINAMAPUNGUFU
Next articleUWT ILALA YAWATAKA WANAWAKE WASITUMIKE KISIASA
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here