Home LOCAL MLIPUKO WA UINJILISTI WAZINDULIWA DODOMA

MLIPUKO WA UINJILISTI WAZINDULIWA DODOMA

Katibu wa Jimbo la Kati mwa  Tanzania  (CTF) Mchungaji  Festo Mng’ong’o  kutoka Kanisa la Waadventista Wasabato  akizungumza wakati wa  uzinduzi wa programu ya Mlipuko wa Uinjilisti  katika Kanisa la Chang’ombe Februari 11, 2023 Jijini Dodoma.

Kwaya ya Amani kutoka kanisa la Waadventista Wasabato Chang’ombe wakiimba katika wa  uzinduzi wa programu ya Mlipuko wa Uinjilisti  katika Kanisa la Chang’ombe Februari 11, 2023 Jijini Dodoma.

(PICHA ZOTE NA KANISA LA CHANG’OMBE)

Na: Mwandishi wetu- Dodoma.

Waumini wa dini ya Kikristo nchini wamehimizwa kushiriki katika kazi ya Mungu ya kueneza injili Ulimwenguni kote ili watu wamjue Mungu na kubadilisha mienendo yao mibaya pamoja na kuwa na jamiii yenye maadili mema.

Kauli hiyo imetolewa na Katibu wa Jimbo la Kati mwa  Tanzania (CTF) Mchungaji  Festo Mng’ong’o  kutoka Kanisa la Waadventista Wasabato  wakati akizindua programu ya Mlipuko wa Uinjilisti  ambayo imeanza Februari 11 mwaka 2023 katika Kanisa la Chang’ombe SDA  inayolenga kila muumini kuleta mshiriki mpya kanisani hadi ifikapo 2025.

Amesema kila muumini ana wajibu wa kufanya kazi ya Mungu kulingana na talanta aliyopewa  ili kuvuta watu wengi kufahamu Mungu na kurekebisha tabia zisizo njema.

“Haya ni maandalizi ya wakazi wa Dunia kumlaki Yesu anapokuja kwa sababu ishara zote , matukio yanayotokea yanaonyesha kwamba Dunia imefikia mwisho hivyo  wito wa Mungu ni kila jamaa, kabila afikiwe na ujumbe huu na kanisa limejipanga kufanikisha hilo,”Amesema Mchungaji Mng’ong’o.

Naye  Mzee wa Kanisa la Waadventista Wasabato Miyuji, Lameck Barinda ameahidi kuhamisha waumini katika kanisa lake kuhakikisha kila muumini anafanya sehemu yake kwa kufundisha watu wengine habari njema wakati wa kujiandaa kumpokea Yesu anapokuja mara ya pili.

“Kanisa la Miyuji tumejipanga kufanya ushuhudiaji nyumba kwa nyumba na tuna mpango wa kufanya mikutano mitatu ya injili kwa mwaka huu,”Ameeleza Barinda.

Kwa upande wake Paul Samson ambaye ni Mzee wa Kanisa la Waadventista Wasabato Chang’ombe akaeleza kuwa kama viongozi wa kanisa hilo ni kuwajibika kuwaleta watu kwa Yesu huku akiwasihi  waumini kujihusisha kila mmoja kwa wakati wake kufanya kazi ya Mungu.

“Viongozi tumejipanga kuwatembelea waumini walioyumba kiimani na tunawatia moyo wumini kila mmoja mahali alipo iwe ni kazini, maeneo ya biashara  au nyumbani kazi kubwa ni kuwaongoza watu kumjua MUngu,”Amefafanua Mzee Paul.

Aidha Mzee wa  Kanisa la Waadventista Wasabato  Veyula, Benjamin Yonathan akabainisha kuwa kanisa limejipanga kufanya mikutano miwili ya injili itakayohusisha wakazi wote wa maeneo hayo kwa pamoja kujifunza neno la Mungu.

“Naamini  ndilo kusudi tuliloitiwa  na Mungu kueneza injili, tunaamini kazi yake itakwenda mbele na ushindi utapatikana kwa kila kundi watoto, wanakwaya, wanawake,  vijana pamoja na wenye ulemavu,”Amesema Mzee Yonathan.

Programu hiyo ya Mlipuko wa Uinjilisti imeanza rasmi Februari 11 mwaka 2023 hadi kufikia 2025 ikiwa na kaulimbiu isemayo “ Jihusishe Yesu Anakuja”

MWISHO.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here