Waziri wa Fenda na Mipango, Mhe.Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akisalimiana na Katibu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Bw. Peter Mathuki kabla ya kuanza kwa Mkutano wa 43 wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), unaofanyika Jijini Bujumbura, Burundi.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (kushoto) na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Lawrence Tax (Mb) wakipitia nyaraka mbalimbali wakayti wa Mkutano wa 43 wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), uliofanyika Jijini Bujumbura, Burundi. Wa tatu kushoto ni Naibu Waziri wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi– Sekta ya ujenzi, Mhe. Mha. Godfrey Kasekenya (Mb).
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bi. Amina Khamis Shaaban akifuatilia Mkutano wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika Jijini Bunjura nchini Burundi. Kushoto kwa Bi. Amina ni Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Joseph Edward Sokoine na anayefuatia ni Naibu Waziri wa Katika na Sheria Mhe. Geoffrey Mizengo Pinda (Mb).
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akiwa na Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Dkt. Yamungu Kayandabila wakiwasili katika Hotel club du lac Tanganyika kuhudhuria Mkutano wa 43 wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika Jijini Bujumbura nchini Burundi.(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-WFM-Bujumbura)
Na: Ramadhani Kissimba, Bujumbura -Burundi
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) ameshiriki katika Mkutano wa 43 wa kawaida wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika Jijini Bunjura, Burundi. Mkutano huo ambao umefanyika baada ya miaka nane (8) toka ulipofanyika kwa mara ya mwisho nchini Burundi umeshirikisha Mawaziri wanaosimamia masuala ya Afrika Mashariki na ushirikiano wa Kikanda pamoja na Mawaziri wenye agenda zinazojadiliwa na Baraza hilo.
Awali kabla ya Mkutano huo kulitanguliwa na vikao vya Wataalamu na Makatibu Wakuu kutoka katika nchi wanachama vilivyofanyika kuanzia tarehe 19 – 22 Februari, 2023 ambao walipitia agenda na mapendekezo mbalimbali ya Jumuiya. Aidha wataalamu hao walipitia taarifa ya utekelezaji wa maazimio yaliyofikiwa kwenye vikao vilivyopita katika maeneo ya biashara, forodha, miundombinu, ulinzi na usalama, sheria, utalii, ajira, utawala na fedha.
Dkt. Nchemba ameshiriki Mkutano huo pamoja na ujumbe wa Tanzania ulioongozwa na Waziri wa Mambo ya nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe.Dkt. Stergomena Lawrence Tax (Mb), ambapo watajadili na kupitisha mapendekezo ya agenda mbalimbali ikiwa ni pamoja na umuhimu wa kuitangaza lugha ya Kiswahili kwa kuanzisha vituo vya utamaduni wa lugha hiyo katika Balozi za nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki na kutoa muelekeo wa kuanza kutumika kwa lugha ya Kiswahili na Kifaransa katika uendeshaji wa shughuli rasmi za Jumuiya.
Mkutano wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki ambao ulikuwa chini ya Uenyekiti wa Burundi na kuhudhuriwa na wajumbe kutoka nchini Tanzania, Burundi, Kenya, Uganda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Rwanda na Sudan Kusini umemalizika tarehe 23 Februari, 2023 na maazimio na agenda zilizopitishwa zitawasilishwa katika mkutano wa Marais wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa ajili ya kuridhia utekelezaji wake.