Waziri wa Nishati January Makamba (kushoto mwenye suti nyeusi) akikabidhi kibali cha ujenzi wa Bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki kwa Mwenyekiti wa Bodi ya EWURA Prof. Marc Mwandosya (kulia) katika hafla iliyofanyika leo Februari 21,2023 Jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Nishati January Makamba akizungumza mara baada ya kukabidhi kibali cha ujenzi wa Bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki kwa Mwenyekiti wa Bodi ya EWURA Jijini Dar es Salaam
Mwenyekiti wa Bodi ya EWURA Prof. Marc Mwandosya akizungumza katika hafla alipokuwa akitoa hotuba yake kumkaribisha Mgeni rasmi kuzungumza.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Amos Makalla akitoa neno la utangulizi katika hafla hiyo.
Naibu Mkurugenzi wa Kampuni ya EACOP Tanzania Bi. Wendy Brown akizungumza kuelezea utekelezaji wa Mradi huo.
Mkurugenzi Mkuu wa EWURA Dkt James Andilile akizungumza Katika hafla hiyo muda mfupi kabla ya zoezi la kukabidhi kibali cha Ujenzi wa Bomba la Mafuta Jijini Dar es Salaam.
(PICHA NA: HUGHES DUGILO).
Picha mbalimbali za viongozi na wadau walioshiriki katika Mkutano huo.
Na. Hughes Dugilo, DSM.
Serikali kupitia Wizara ya Nishati imekabidhi kibali cha ujenzi wa Bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki kwa kampuni ya EACOP Tanzania LTD kwaajili ya kuanza Ujenzi wa Bomba hilo kutoka Mtukula hadi Chongoreani Mkoani Tanga.
Akizungumza Katika hafla ya makabidhiano hayo iliyofanyika leo Februari 21,2023 Jijini Dar es Salaam Waziri Wa Nishati Januari Makamba amesema kuwa mchakato wa kukabidhi kibali hicho umezingatia masuala ya utunzaji wa mazingira pamoja na haki za Binadamu
Aidha amebainisha kuwa tayari mradi umeanza kutekelezwa kwa kulipa fidia kwa wakati katika maeneo yaliyopitiwa na mradi huo katika mikoa minane ambapo kaya zaidi ya 9800 wameshalipwa fidia.
“Tayari tumelipa fidia shilingi bilioni 29, na mradi huu umeanza kutekelezwa katika baadhi ya maeneo, mfano kununua vifaa, kuanza ujenzi wa vituo vya kuhifadhia mafuta Mkoani Tanga. kwa hiyo tunatarajia mradi huu ulete ajira nyingi za moja kwa moja lakini pia ajira za kutoa huduma kama vile hoteli, hivyo Watanzania wachangamkie fursa hiyi” amesema Waziri Makamba.
Aidha ameitaka Malaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji ( EWURA) ambayo imepewa asilimia 15 ya usimamizi wa mradi huo kwenye kampuni ya EACOP kuhakikisha inatangaza fursa zilizopo pamoja na kusimamia ipasavyo sheria ya Local Content kwa kuhakikisha wazawa wanapata fursa mbalimbali zitokanazo na mradi huo.
Pia kuhakikisha wazawa wanafaidika na mradi huo kwa kutoa fursa ya kushiriki katika ujenzi wa Bomba hilo.
Awali akizungumza Katika hafla hiyo Mkurugenzi Mkuu wa EWURA Dkt James Andilile ameeleza kuwa Kampuni ya EACOP imepewa zabuni hiyo kutokana na kukidhi masharti ya kimkataba ikiwemo kuzingatia masuala ya utunzaji wa mazingira, Athari za kiubinadamu, pamoja na uwezo wa kitaalamu na kifedha kwa ajili ya kutekeleza mradi.
“Ujenzi huu wa kipande cha kutoka Mtukula hadi Chongoreani Mkoani Tanga una urefu wa kilomita 1147 , sisi kama EWURA tuna matumaini kwamba kampuni ya EACOP TZ itaendelea kuzingatia yote tuliyokubaliana kabla na baada ya ujenzi wa Bomba hili” amesema Dkt Andilile.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Tanga Omary Mgumba akizungumza kwa niaba ya wakuu wa mikoa wenzake ambapo Mradi huo umepita amesema watahakikisha wanasimamia vema miundombinu ya mradi huo kwa kutumia Jeshi la Akiba huku wakiiomba Serikali kujenga vituo vya polisi katika vituo vya kuhifadhia mafuta ghafi ili kuhakikisha ulinzi na usalama unakuwepo wakati wote wa Ujenzi na baada ya kukamilika.
Kwa upande wake Naibu Mkurugenzi wa Kampuni ya EACOP Tanzania ambayo imekabidhiwa Kibali cha ujenzi wa mradi huo Bi. Wendy Brown amesema kuwa Kampuni hiyo itahakikisha inazingatia makubaliano ya mkataba na kwamba itahakikisha ujenzi huo una kamilika kwa wakati.
Mradi wa Bomba la Mafuta ghafi ambao umepata Kibali rasmi leo unatekelezwa katika mikoa nane ambayo ni pamoja na Tanga, Manyara, Dodoma, Singida, Tabora, Shinyanga, Geita na Kagera, ambapo unatarajiwa kutoa fursa mbalimbali za kiuchumi kwa wananchi waishio Katika mikoa hiyo.