Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Dkt. Ashatu Kijaji akizungumza katika Mkutano na waandishi wa habari uliofanyika leo Februari 17, 2023 Jijini Dar es salaam juu ya Kongamano la Kimataifa la Biashara kati ya Tanzania na Jumuiya ya Ulaya litakalofanyika kwa siku mbili Februari 23 na 24 Jijini humo. (Kushoto) ni Naibu Mkuu wa Jumuiya ya Ulaya nchini Tanzania Emilio Rossetti, na (kulia), ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Uwekezaji Viwanda na Biashara, Ali Gugu.
Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Dkt. Ashatu Kijaji akifafanua jambo alipokuwa akijibu maswali mbalimbali ya waandishi wa habari (hawamo pichani) katika Mkutano huo.
Naibu Mkuu wa Jumuiya ya Ulaya nchini Tanzania Emilio Rossetti, (kushoto) akiteta jambo na Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Dkt. Ashatu Kijaji (kulia) muda mfupi kabla ya kuanza kwa mkutano huo.
Naibu Mkuu wa Jumuiya ya Ulaya nchini Tanzania Emilio Rossetti, (kulia) akifafanua jambo alipokuwa akizungumza katika Mkutano huo Leo Februari 17,2023 Dar es Salaam.
Baadhi ya wadau na waandishi wa habari waliohudhuria kwenye Mkutano huo.
Mwakilishi wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania, (TPSF) Kinanasy Seif (kulia) akizungumza katika Mkutano huo.
(PICHA NA: HUGHES DUGILO)
Na: Hughes Dugilo, DAR ES SALAAM.
Tanzania inatarajia kuwa mwenyeji wa Kongamano la Kimataifa la Biashara kati yake na Nchi za Umoja wa Ulaya linalotarajiwa kufanyika kuanzia Februari 23 na 24, 2023 katika Ukumbi wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNlCC) Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika Mkutano na waandishi wa habari uliofanyika leo Februari 17, 2023 Jijini Dar es salaam, Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Dkt. Ashatu Kijaji amesema kuwa Kongamano hilo limeandaliwa na Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara kwa kushirikiana na Umoja wa Ulaya pamoja na Sekta Binafsi ya Tanzania (TPSF).
Dkt. Kijaji amesema kuwa Kongamano hilo litawaakutanisha zaidi ya wafanyabiashara 600 kutoka katika nchi zinazounnda jumuiya ya Ulaya.
“Kongamano hili linalenga kuwaunganisha washiriki hao ili kuwawezesha kubadilishana uzoefu, kushirikiana na watoa maamuzi na kukutana na wawekezaji wanaofaa pamoja na kujenga uelewa kuhusu fursa za uwekezaji zilizopo kwa sekta ya umma na binafsi ambapo, Hati za Makubaliano mbalimbali ya Uwekezaji baina ya Tanzania na Nchi za Umoja wa Ulaya zitatiwa saini” ameeleza Dkt. Kijaji.
Aidha Dkt. Kijaji amesema kuwa Kongamano hilo litahudhuriwa na Mawaziri nane (8) kutoka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na Mabalozi sita (6) wa Tanzania katika nchi za Umoja wa Ulaya ambao watashiriki katika vikao vya majadiliano kati ya Serikali na Biashara.
Akizungumzia mashirikiano ya kibiashara yaliyopo kati ya Tanzania na Ulaya, Waziri Kijaji amesema kuwa kwa mwaka 2021 Tanzania iliuza bidhaa zenye thamani ya Euro milioni 456 ambazo zilijumuisha bidhaa za kilimo na kununua bidhaa zenye thamani ya Euro milioni 856 ambazo zilijumuisha madawa, ndege mashine.
Aidha Dkt. Kijaji ametoa mwito kwa Wafanyabiashara na wawekezaji kutoka Tanzania kutumia vizuri fursa ya uwepo wa Kongamano hilo kuendeleza na kukuza biashara zao kwa kujifunza mbinu mpya za kibiashara, kupata wabia na masoko ya bidhaa zao nje ya nchi.
“Ninatarajia kuona Kongamano hili la Biashara la kwanza kuwa fursa ya kuvutia wawekezaji, teknolojia na utalaamu katika nchi yetu na kuvutia biashara na uwekezaji kutoka duniani kote katika sekta za nishati, madini na kilimo endelevu. Hivyo tunatarajia hati za makubaliano zitakazotiwa saini zitaendeleza na kukuza biashara kati ya Tanzania na Umoja wa Ulaya, zitaongeza ajira kwa vijana na zitachangia katika ukuaji wa uchumi wa nchi yetu” amesema.
Kwa upande Naibu Mkuu wa Jumuiya ya Ulaya nchini Tanzania Emilio Rossetti amesema kuwa katika Kongamano hilo kutasainiwa mikataba kati ya Benki ya Uwekezaji ya Jumuiya ya Ulaya na Taasisi za kifedha za Tanzania.
Amesisitiza kuwa Wafanyabiashara wa Tanzania wana fursa za kunufaika na soko la Ulaya lenye watu zaidi ya milioni 400.
“Wafanyabiashara wa Tanzania wana fursa za kunufaika na soko la watu zaidi ya milioni 400 katika nchi zinazounda jumuiya” amesema Rossetti
Naye mwakilishi wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania, (TPSF) Kinanasy Seif akizungumza katika Mkutano huo ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji nchini.
Aidha amebainisha kuwa mpaka sasa jumla ya wafanyabiashara 250 tayari wamethibitisha kushiriki katika kongamano hilo.