Na: Ahmed Sagaff – MAELEZO
Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) limevitaka vyombo vya habari nchini kuomba radhi na kufuta picha za vijana katika habari zao zinahusu takwimu za vijana 147 waliobainika kuwa na Virusi Vya UKIMWI (VVU) mara baada ya kupimwa na jeshi hilo walipokuwa wakiandikishwa kwenye mafunzo kuanzia mwaka 2018/2019 hadi 2020/2021.
Akizungumza leo jijini Dodoma, Mkuu wa Tawi la Utawala la JKT, Brigedia Jenerali Hassan Mabena amesema vijana waliooneshwa kwenye picha hizo sio waliobainika kuwa na VVU.
“JKT inaamini kuwa kitendo hicho ni cha udhalilishaji wa utu wa mwanadamu na kutumia picha zisizohusiia katika habari hiyo iliyoripotiwa bungeni Februari 3, 2023 ni cha ukosefu wa maadili ya vyombo vya habari na kwamba uhuru wa vyombo vya habari haukutumika ipasavyo,” ameeleza Brigedia Jenerali Mabena.
Sambamba na hilo, Brigedia Jenerali amekumbusha kwamba takwimu hizo zilipatikana kwa wahitimu wa kidato cha sita pindi walipotaka kujiunga na JKT na kwamba jeshi hilo limewapa mafunzo chini ya uangalizi maalumu huku wakipatiwa ushauri nasaha na tiba.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) na Msemaji Mkuu wa Serikali, Ndg. Gerson Msigwa amesema Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imeandaa mafunzo kwa ajili ya wanahabari ili kukumbushana mambo ya msingi kuhusu taaluma ya uandishi wa habari.