· CTI yaomba Serikali ilinde viwanda vya ndani
Na: Mwandishi Wetu
SHIRIKISHO la Wenye Viwanda Nchini (CTI), limeiomba serikali kupunguza au kuondoa kodi kwa malighafi zinazotoka nje ya nchi kwaajili ya kusaidia uzalishaji wa bidhaa mbalimbali hapa nchini na kuzitoza kodi stahiki zile bidhaa zinazotoka nje ya nchi.
Hayo yamesemwa jinini Dar es Salaam Mkurugenzi Mtendaji wa (CTI), Leodeger Tenga, wakati wa kikao baina ya shirikisho hilo na Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Dk. Ashatu Kijaji na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba.
“Lazima tuwe waangalifu sana kwa viwanda vyetu vya ndani, unaposema soko huru unaweza kukuta wewe unageuzwa soko la bidhaa za wenzako kama hukutengeneza mazingira amzuri kwa watu wako wa ndani kuzalidha bidhaa nzuri na kwa bei nafuu,” alisema
Aalisema mkutano umekuwa na manufaa makubwa kutokana na wafanyabiashara hao kupata fursa ya kuelezea yanayowakwanza kutoka kwa mawaziri wawili kuhusu mazingira ya biashara.
Alisema lengo la mkutano huo ni kuhakikisha kwamba wanajenga mazingira wezeshi ya ufanyaji mzuri wa biashara unaovutia uwekezaji na wawekezaji wanapokuja wakute mazingira mazuri.
“Pia imekuwa nafasi nzuri kwa wenye viwanda na wafanyabiashara kuishukuru serikali kwa mambo mema ambayo imefanya ambayo yako mengi na pia kukumbushana mengine ambayo bado yanahitaji kufanyiwa kazi,” alisema
Alisema changamoto nyingi zilizokuwa zikiwakabili wafanyabiashara zimefanyiwa kazi na serikali lakini aliomba kero ziliozosalia zifanyiwe kazi kwa haraka ili kuvutia uwekezaji kwa wingi kutoka nje.
Aliwataka wazalishaji wa Tanzania kujitahidi kuzalisha bidhaa bora na zenye unafuu ili ziweze kuvutia masoko mengi na makubwa kwa Afrika Mashariki na kwingineko duniani.
“Kama nchi imeshafanya maamuzi ya msingi ya kuingia kwenye soko huru la Afrika na tuko pia kwenye soko la Afrika Mashariki hivyo ili tuweze kushindana lazima tuzalishe bidhaa bora vinginevyo tutageuka soko la wenzetu kwa hiyo hakuna namna lazima tuzalishe bidhaa bora ili tushindane,” alisema
“Lazima tushindane kwa mambo mawili, tushindane kwa ubora na tushindane kwa bei. Wakati mwingine bidhaa zinaongezeka bei kutokana na changamoto za usafiri au za kikodi sasa yale ya kikodi tayari mapendelezo yetu ya kikodi yameshawasilishwa serikalini,” alisema.
Wakati huo huo, Serikali imetangaza kuwa kuanzia Julai Mosi mwaka huu itaanza kupeleka aina 10 za bidhaa katika Soko la Huru la Biashara Afrika ambalo Tanzania ni mwanachama.
Akizungumza kwenye mkutano huo, Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Dk. Ashatu Kijaji alisema Tanzania ni miongoni mwa nchi saba za mwanzo zilizopewa kipaumbele cha kupeleka bidhaa kwenye soko hilo hivyo kuwataka wafanyabiashara wachangamkie fursa hiyo adimu.
“Tumeshakutana Januari na leo ni kikao chetu cha tatu kukutana na wadau wazalishaji wa viwanda na wafanyabiashara kuelimishana kuhusu kinachohitajika kwenye eneo huru la biashara Afrika,” alisema
“Tayari tumeshapata bidhaa ya kwanza itakayotangulia ambayo ni kahawa na hatutapeleka ikiwa ghafi tutapeleka iliyokwishachakatwa (finished product),” alisema Waziri Kijaji
Alitaja bidhaa nyingine itakayopelekwa kwenye soko hilo kuwa ni marumaru zinazozalishwa hapa nchini na kwamba serikali imeshajadiliana na wazalishaji wa bidhaa hiyo na wako tayari kusafirisha.
“Kuna bidhaa zingine bado tunajadiliana na wazalishaji sitaziweka wazi leo lakini kwa ujumla tuko tayari kuingia na aina 10 za bidhaa kwenye soko hili kuanzia Julai Mosi mwaka huu tunaendelea kuelezana kinachohitajika na vitu vya kuzingatia kutoka kwa wazalishaji wetu wa ndani,” alisema
“Niwahakikishie wazalishaji wetu wa viwandani na wale wa bidhaa zingine kwamba serikali iko tayari na vikao hivi ni endelevu tutaendela kupeana taarifa na kama alivyosema mheshimiwa Rais kwamba tusiwe wasindikizaji kwenye hili soko,”alisema
Mwisho.