Jukwaa la wahariri Tanzania (TEF) limemuomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan kuingilia kati mchakato wa Marekebisho ya Sheria ya Huduma za Habari (MSA 2016) baada ya Muswada wa sheria hiyo kushindikana kuingizwa Bungeni katika Mkutano wake wa kumi unaondelea Jijini Dodoma.
Taarifa iliyotolewa Februari 8, 2023 Jijini Dar es Salaam, na TEF inasema kuwa Jukwaa hilo limepokea kwa mshituko na masikitiko makubwa kauli ya Serikali kupitia kwa Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa kuwa Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Huduma za Habari (MSA 2016) umeshindikana kuingizwa Bungeni kutokana na ripoti nyingi za Kamati za Kisekta za Bunge.
“Mwanzo tuliahidiwa muswada wa mabadiliko ungeingizwa Bungeni mwaka 2022 katika vikao vya Februari, wakasema Aprili, baadaye Septemba, ikasogezwa Novemba, lakini kote huko hakuna kilichotekelezwa”
“Zamu hii tuliweka matumaini makubwa na hasa baada ya Waziri Nape kutangaza hadharani kuwa amewasilisha mapendekezo Ofisini kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na kuwa Februari hii muswada huu ungeingizwa Bungeni”
Kutokana na hali hiyo wamemuomba Rais Samia kuinusuru hali hiyo na kwamba hawajafurahishwa na mwenendo huo katika suala la mabadiliko ya Sheria ya Huduma za Habari (MSA, 2016), na kuomba kukutana naye wakiamini kuwa mkutano huo utawakwamua walipokwama.
“Tunaomba Rais Samia anusuru hali hii katika suala la mabadiliko ya Sheria ya Huduma za Habari (MSA, 2016). Tunaomba tukutane na Mhe. Rais Samia, tukiamini mkutano huo utatukwamua tulipokwama”