Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akizungumza na waandishi wa habari leo kuhusu kumalizika kwa kambi maalum ya matibabu na upimaji wa magonjwa ya moyo ya siku tano iliyofanyika katika Hospitali ya Rufaa Mnazi Mmoja Zanzibar. Kulia kwake ni Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Rufaa Mnazi Mmoja Zanzibar Dkt. Muhiddin Abdi Mahmoud.
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Rufaa Mnazi Mmoja Zanzibar Dkt. Muhiddin Abdi Mahmoud akizungumza na waandishi wa habari leo kuhusu kumalizika kwa kambi maalum ya matibabu na upimaji wa magonjwa ya moyo iliyofanyika katika Hospitali ya Rufaa Mnazi Mmoja Zanzibar. Katika kambi hiyo jumla ya watu 718 walipata huduma za upimaji na matibabu ambapo 75 walipewa rufaa ya kwenda kutibiwa JKCI.
Watu 718 wafanyiwa uchunguzi na matibabu ya moyo Zanzibar
Na Mwandishi Maalum – Zanzibar 27/1/2023 Jumla ya watu 718 wamepata huduma za upimaji na matibabu ya moyo katika kambi maalum ya matibabu iliyofanywa na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao wa
Hospitali ya Rufaa Mnazi Mmoja Zanzibar.
Hayo yamesemwa leo na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge wakati wa kufunga kambi maalum ya upimaji na matibabu ya moyo ya siku tano iliyofanyika katika Hospitali ya Mnazi Mmoja Zanzibar.
Dkt. Kisenge alisema kati ya watu waliofanyiwa upimaji na matibabu ya moyo watu wazima walikuwa 627 na watoto 91, waliokutwa na matatizo yaliyohitaji matibabu ya kibingwa na kupewa rufaa ya kwenda kutibiwa katika Taasisi hiyo walikuwa 75.
“Tumefanya upimaji kwa kushirikiana na wenzetu wa Hospitali ya Rufaa Mnazi Mmoja Zanzibar, wananchi wamejitokeza kwa wingi kupima afya zao kwa kufanya hivi wameweza kujijua kama wana matatizo ya moyo au la na kwa ambao wamekutwa na matatizo wataweza kuanza matibabu mapema”,
“Wananchi waliofika katika upimaji walipimwa bila malipo yoyote yale urefu, uzito,shinikizo la damu (BP), kiwango cha sukari mwilini, vipimo vya kuangalia jinsi mfumo wa umeme wa moyo unavyofanya kazi (Electrocardiogram- ECG) na moyo unavyofanya kazi (Echocardiogram – ECHO)”, alisema Dkt. Kisenge.
Dkt. Kisenge ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo alisema kulikuwa na wataalamu wa lishe ambao wametoa elimu ya lishe bora ambayo imewapa wananchi uelewa na kufuata mtindo bora wa maisha ambao utawasaidia kuepukana na magonjwa ya moyo ambayo ni moja ya magonjwa yasiyoambukiza na yanaweza kuepukika kwa kufuata mtindo bora wa maisha na ushauri wa kitaalamu.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Rufaa Mnazi Mmoja Zanzibar Dkt. Muhiddin Abdi Mahmoud aliishukuru Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete kwa kutuma wataalamu wake ambao wametoa huduma ya upimaji na matibabu kwa wananchi wa visiwa hivyo.
Dkt. Mahmoud alisema wamejipanga kuhakikisha madaktari bingwa wa moyo wanakuwepo katika Hospitali hiyo kila mwezi ili wananchi waweze kupata huduma hiyo na kuwapunguzia safari ya kwenda kufuata huduma ya kibingwa ya matibabu ya moyo Dar es Salaam.
Akizungumzia jinsi ya kuepukana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza yakiwemo ya moyo Dkt. Mahmoud alisema wananchi wafuate mtindo bora wa maisha kwa kula vyakula bora, kufanya mazoezi, kuacha kutumia bidhaa aina ya tumbaku na
kutokunywa pombe kupitiliza.
Kwa upande wa wananchi waliopata huduma ya upimaji na matibabu ya moyo waliishukuru Serikali kwa kuwapatia huduma yamatibabu na kusema kuwa imewasaidia kujua afya zao za moyo zikoje pia ushauri wa lishe walioupata utawasaidia kula vyakula bora na kutunza mioyo yao.
Zuhura Hakim alisema aligundulika kuwa na tatizo la kutanuka kwa moyo mwaka 2020 alipokuwa na mimba ya mtoto wa tatu baada ya kutumia dawa kwa muda wa miaka mitatu amepona na daktari amemwambia asitumie dawa
tena.
“Ninashukuru sana kwa huduma hii kwani baada ya kufanyiwa vipimo nimekutwa tatizo la kutanuka kwa moyo limeisha moyo wangu umerudi katika hali yake ya kawaida, ninawasihi kina mama wenzangu wanaokutwa na matatizo haya wakati wa ujauzito wasikate tamaa watumie dawa na kufuata ushauri wa wataalamu kama nilivyofanya mimi”,
alisema Zuhura. Ibrahim Soud alishukuru kwa huduma aliyoipata na kuiomba Serikali ihakikishe huduma kama hiyo ya upimaji na matibabu ya moyo ya kibingwa inapatikana mara kwa mara.
Mwisho.