Waziri Bashe ametoa agizo hilo leo Januari, 2023 wakati wa ziara ya kikazi Mkoani Ruvuma alipokuwa akipokea taarifa ya Maendeleo ya Sekta ya Kilimo ikiwa ni siku ya kwanza ya ziara ya siku mbili mkoani humo.
Mhe. Bashe amesema, Vyama Vikuu vya Ushirika Mkoani humo vimekuwa vinaratibu upatikanaji wa mbolea na pembejeo za Korosho, Tumbaku na Kahawa kwa wakulima; sasa wajipange waanze pia kusambaza mbolea za mazao mengine kama vile Mahindi, Soya na Mbaazi.
“Kuanzia mwakani nataka kuona vyama hivi vinaratibu upatikanaji wa mbolea za mazao mengine ili wakulima waweze kupata mbolea kwa wakati na kwa urahisi kisha kuongeza tija katika uzalishaji,” Waziri Bashe amesisitiza.
Aidha, Waziri Bashe ameziagiza Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC) na Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) kufanya kazi kwa kushirikiana na kuhakikisha mbolea inawafikia wakulima kupitia Vyama vya Ushirika.
“Mkifanikiwa kupitishia Mbolea katika Vyama Vikuu sitegemei kusikia kelele kutoka kwa wakulima kuhusu mboelea na wakati Tume ya Maendeleo ya Ushirika mmesambaa kila mikoa,” Waziri Bashe alisisitiza.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Ruvuma, Mhe. Odo Mwisho amepongeza jitihada za Wizara za kuagiza Mbolea kuwafikia wakulima kupitia Vyama Vikuu vya ushirika na kubainisha itasaidia kupunguza usumbufu kwa mkulima mmoja mmoja kufuata mbolea katika vituo vilivyopo Mijini.
Amesema wakulima wanatoka maeneo ya mbali kufuata Mbolea kwa wakala wa usambazaji hali inayosababisha kutumia muda mwingi katika foleni ya ununuzi wa mbolea hiyo, hivyo anaamini ikipitia katika Vyama Vikuu kila mkulima atapata mbolea yake kwa muda sahihi na karibu na maeneo ya uzalishaji.
Pia, Mhe. Mwisho ameiomba Serikali katika mgao wa ujenzi wa maghala ishirini mapya Ruvuma ambao unategemea kuanza kujengwa hivi karibuni basi uweze kuzingatia uhitaji wa maeneo na si kurundika maeneo ambayo hayana uhitaji.
“Yapo maeneo ambayo maghala yaliyopo yanajitosheleza, nakuomba Mheshimiwa Waziri katika ujenzi wa maghala hayo yajengwe sehemu ambazo kweli zinauhitaji ili kuepusha utitiri na mlundikano wa Maghala sehemu moja,” amesema Mhe. Mwisho.