Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Tumaini Nagu na Kansela wa Uchumi na Biashara kutoka Ubalozi wa China Nchini Tanzania Chu Kun wakisaini muhtasari wa taarifa ya upembuzi yakinifu ya ujenzi na upanuzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) katika eneo la Mloganzila lililopo wilayani Ubungo jijini Dar es Salaam.
Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Tumaini Nagu pamoja na Kansela wa Uchumi na Biashara kutoka Ubalozi wa China nchini Tanzania Chu Kun wakionesha muhtasari wa taarifa ya upembuzi yakinifu ya ujenzi na upanuzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) katika eneo la Mloganzila mara baada ya kusaini muhtasari huo leo katika ukumbi wa Taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam.
Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Tumaini Nagu akielezea namna ambavyo Serikali kupitia Wizara ya Afya imejipanga kuboresha miundombinu ya afya wakati wa kusaini muhtasari wa taarifa ya upembuzi yakinifu ya ujenzi na upanuzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) katika eneo la Mloganzila lililopo wilayani Ubungo jijini Dar es Salaam.
Mkurugezi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akizungumza wakati wa kusaini muhtasari wa taarifa ya upembuzi yakinifu ya ujenzi na upanuzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) katika eneo la Mloganzila lililopo wilayani Ubungo jijini Dar es Salaam.
Picha Na: Khamis Mussa
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya watu wa China zimesaini muhtasari wa taarifa ya upembuzi yakinifu ya ujenzi na upanuzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) katika eneo la Mloganzila lililopo wilayani Ubungo.
Muhtasari huo umesainiwa leo Jijini Dar es Salaam na Kansela wa Uchumi na Biashara kutoka Ubalozi wa China nchini Tanzania Chu Kun pamoja na Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Tumaini Nagu kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Prof. Abel Makubi.
Akizungumza na waandishi wa Habari wakati wa kusaini muhtasari huo Mganga mkuu wa Serikali Prof. Tumaini Nagu alisema kwa sasa JKCI imekuwa ikitoa huduma kwa wagonjwa wa moyo wa ndani na nje ya nchi hivyo kuongeza idadi ya watu wanaotibiwa katika Taasisi hiyo inayopelekea uhitaji wa upanuzi wa Taasisi.
“Huduma za matibabu na upasuaji wa moyo zimeendelea kuhitajika kwa wingi kwasababu magonjwa yasiyo ambukiza yameendelea kuongezeka hivyo kuhitaji eneo la kutosha ili kuwapatia wagonjwa wote nafasi ya kupata huduma bobezi za matibabu ya moyo”,.
“Eneo ilipo Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) ni finyu, hivyo Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu alipotembelea nchini China mwaka 2018 na kukutana na Waziri wa Afya wa nchi hiyo alitoa ombi la kushirikiana nao ili kwa pamoja tuweze kupanua wigo wa JKCI”, alisema Prof. Tumaini.
Prof. Tumaini alisema JKCI itakapofanikiwa kupanua wigo na kupata eneo la kutosha kuwahudumia wagonjwa wa moyo itaenda kuongeza ufanisi katika kutoa huduma na kwenda kuwa kituo cha umahiri katika kutoa huduma za matibabu na upasuaji wa moyo”,
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alisema mradi wa kuongeza jengo la matibabu ya moyo eneo la Mloganzila utaenda kupunguza msongamano wa wagonjwa kwani sasa Taasisi hiyo inahudumia wagonjwa wa nje 400 kwa siku.
“Jengo letu limekuwa dogo kutokana na mahitaji ya matibabu kuongezeka hivyo tutakavyoenda kujenga Mlonganzila naamini tutakidhi mahitaji ya wagonjwa wetu katika kutoa huduma za matibabu na upasuaji wa moyo”,
Sasa hivi Taasisi yetu ya moyo inapokea wagonjwa zaidi ya 50 kwa mwezi kutoka nchi mbalimbali Duniani ambapo wagonjwa hao wengi wao hutoka nchini Kenya, Visiwa vya Comoro, Malawi, Zimbabwe, Rwanda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na nchi nyinginezo za Ulaya”, alisema Dkt. Kisenge.
Dkt. Kisenge alisema mradi wa ujenzi wa upanuzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete eneo la Mlonganzila unatarajiwa kuanza rasmi mwakani baada ya upembuzi yakinifu wa eneo hilo kumalizika.
Naye Mkuu wa wilaya ya Ubungo Mhe. Kheri James aliishukuru Wizara ya Afya kufikia hatua ya kutimiza malengo makuu yaliyowekwa na Serikali ya Tanzania pamoja na ile ya Jamhuri ya watu wa China.
Mhe. Kheri alisema nchini Tanzania mageuzi makubwa katika sekta ya afya yamefikiwa lakini yameongezeka zaidi kupitia mahusiano ya kidiplomasia yaliyopo baina ya Tanzania na Jamhuri ya watu wa China.
“Mahusiano kati ya Tanzania na China yametusaidia katika ujenzi wa miundombinu, ubadilishanaji wa ujuzi baina ya wataalam wa afya wa Tanzania na China, lakini pia yamesaidia katika usimamizi wa sekta ya afya hivyo kuimarisha huduma za afya na utaalam nchini mwetu”, alisema Mhe. Kheri
Mhe. Kheri alisema wilaya ya Ubungo imekuwa ni sehemu iliyoainishwa katika kutengeneza mji wa kitabibu ambao utasaidia wananchi kupata elimu ya afya, huduma za afya na kuwa kimbilio la utalii wa afya nchini Tanzania.
“Muhtasari wa upembuzi yakinifu uliosainiwa leo kwa ajili ya kupanua huduma za Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete unaenda kuongeza huduma za kibingwa za matibabu ya moyo katika wilaya yetu, nawahakikishia kuwa wilaya ya Ubungo itatoa ushirikiano kwa kila kitakachohitajika kutimiza malengo yaliyowekwa na wizara ili yale tuliyoyapanga yaweze kukamilika kwa wakati”, alisema Mhe. Kheri.