Home LOCAL KAMPENI YA MSAADA WA KISHERIA KUFANYIKA NCHI NZIMA – Dkt. Kazungu

KAMPENI YA MSAADA WA KISHERIA KUFANYIKA NCHI NZIMA – Dkt. Kazungu

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Dkt. Khatibu Kazungu akihutubia katika kikao kazi cha Kamati ya Maandalizi ya Kampeni ya _Mama Samia Legal Aid Campaign_ tarehe 24 Januari, 2023 Jijini Dodoma.

Wajumbe wa Kamati wakimsikiliza Mgeni Rasmi Dkt. Khatibu Kazungu (hayuko pichani) alipokuwa akiwahutubia wakati wa ufunguzi wa Kikao kazi cha kamati hiyo.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na SheriaDkt. Khatibu Kazungu katika Picha ya pamoja na Wajumbe wa Kamati.

Na: William Mabusi -WKS

Serikali imepanga kufanya kampeni ya Msaada wa Kisheria nchi nzima itakayolenga kutoa elimu juu ya masuala mbalimbali yanayohusiana na sheria kwa watanzania wote.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Katibu Mkuu  wa Wizara ya Katiba na Sheria Dkt. Khatibu Kazungu alipokuwa akifungua kikao kazi cha wajumbe wa Kamati ya maandilizi ya kampeni hiyo tarehe 24 Januari, 2023 Jijini Dodoma.

“Wananchi wengi bado hawana uelewa wa kutosha kuhusu masuala ya kisheria hali inayopelekea wengi wao kukosa haki zao, kutokuzipata kwa wakati au kuzipata kwa gharama kubwa sana.” Alisema Dkt. Kazungu.

Kampeni hiyo ambayo imepewa jina la _Mama Samia Legal Aid Campaign_ itatoa elimu ya kisheria kwa wataalam katika ngazi mbalimbali za kijamii na kwa wananchi wote ili kurahisisha taratibu zinazotakiwa kufuatwa wakati wa utoaji wa Haki na pia Haki iweze kutolewa kwa wakati.

Akitaja baadhi ya maeneo ya kuzingatia wakati wa utoaji elimu, Dkt. Kazungu alisema masuala ya ukatili wa kijinsia, mirathi, masuala ya ardhi na haki za binadamu ni sehemu ya maeneo muhimu yanayogusa jamii na yanatakiwa kutafutiwa ufumbuzi kwa haraka sana.

Aidha, Dkt. Kazungu amehimiza ushirikiano miongoni mwa wadau wa Serikali na wasio wa Kiserikali na kuwataka kutumia weredi, uzoefu na ujuzi wao katika utekelezaji wa kampeni hii katika ngazi za kitaifa na kijamii ili kuhakikisha maeneo yote ya nchi yanafikiwa na hivyo kuleta matokeo makubwa kwa haraka.

 “Tunapopanga kutekeleza kampeni hii tuzingatie kwamba imebeba taswira ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa kukubali kutumia jina lake Mhe. Rais ametuamini kuwa tutafanya kazi hiyo kwa uadilifu wa hali ya juu, tutafanya kazi iliyo njema na hivyo kulinda heshima yake kama Kiongozi Mkuu wa Taifa letu.”  Aliongeza Dkt. Kazungu.

Aidha, amesema kampeni hiyo izingatie azma ya Mhe. Rais katika kulinda haki za kikatiba, utawala wa sheria, na haki za binadamu huku akiwaahidi wahiriki kuwa Wizara ya Katiba na Sheria itatoa ushirikiano wa kutosha katika kufikia malengo yaliyowekwa katika kutekeleza kampeni hiyo. 

Kamati hii inayoongozwa  na Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria kama Mwenyekiti na Bi. Lulu Ng’wanakilala Mkurugenzi Mtendaji wa LSF kama Makamu Mwenyekiti imekutana kwa lengo la kuendelea na maandalizi ya kampeni hiyo ikiwa ni pamoja na kubainisha mahitaji, kazi zitakazotekelezwa, na majukumu ya kila mdau.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here