Home BUSINESS KAMATI YA BUNGE YA ARDHI, MALIASILI NA UTALII YAPOKEA TAARIFA YA UTENDAJI...

KAMATI YA BUNGE YA ARDHI, MALIASILI NA UTALII YAPOKEA TAARIFA YA UTENDAJI WA WIZARA YA MALIASILI NA UTALII

Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imepokea taarifa ya Wizara ya Maliasili na Utalii kuhusu Utekelezaji wa Mpango na Bajeti kwa kipindi cha nusu mwaka (Julai-Desemba, 2022) katika kikao kilichofanyika leo jijini Dodoma.

Akizungumza katika kikao hicho Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Ally Juma Makoa (Mb) ameipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kuendelea kutekeleza majukumu yake ipasavyo pia kwa kuendelea kutatua changamoto mbalimbali zinazojitokeza.

“Wizara mnafanya kazi nzuri tunaziona, changamoto zinazoendelea kujitokeza naomba muendelee kuzitatua kwa wakati” Mhe. Makoa amesisitiza.

Aidha, ameitaka Wizara hiyo kufanyia kazi maoni yaliyotolewa na wajumbe wa Kamati hiyo hususani katika eneo la kukabiliana na changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu pamoja na migogoro kati ya wananchi na maeneo yaliyohifadhiwa.

“Katika kutatua na kumaliza migogoro inayotuhusu nashauri tuendelee kutumia busara ili wananchi waweze kuishi kwa amani na kuendelea kushiriki kikamilifu katika shughuli za uhifadhi” Amesisitiza Mhe. Makoa.

Naye, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Mary Masanja ameishukuru Kamati hiyo na kuahidi kufanyia kazi mapendekezo yote yaliyotolewa ili kuikuza Sekta ya Maliasili na Utalii na hatimaye kuongeza pato la Taifa.

Miongoni mwa masuala yaliyojadiliwa ni utekelezaji wa miradi ya maendeleo ikiwamo Mradi wa Usimamizi wa Maliasili na Kuendeleza Utalii Kanda ya Kusini(REGROW), Mradi wa Kukabiliana na Ujangili na Biashara Haramu ya Wanyamapori, Mradi wa Panda Miti Kibiashara, Mradi wa Kuwezesha Mnyororo wa Thamani wa Mazao ya Nyuki(BEVAC), Mradi wa Kuongeza Thamani kwa mazao ya Misitu (FORV AC) na ukamilishaji wa baadhi ya shughuli za Mpango wa Ustawi kwa Maendeleo ya Taifa na Mapambano Dhidi ya UVIKO-19.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here