Menejimenti ya Chuo cha Misitu Olmotonyi imetakiwa kubuni mikakati mipya ya kujiongezea mapato ili kuongeza udahili wa wanafunzi, motisha kwa wafanyakazi pamoja na kuzalisha mazao yatokanayo na misitu zikiwemo fenicha zenye ubora wa hali wa juu
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja ameyasema hayo leo katika kikao kilichofanyika kwenye ukumbi wa chuo hicho Jijini Arusha ambapo amesema kuna haja ya kukiboresha chuo hicho ili kiweze kuleta tija kwa Taifa.
“Moja ya kazi ya kufanya ni kuendelea kubuni vyanzo vya mapato lakini pia ni lazima muwe na maandiko mahususi yanayojenga hoja kuwafanya wanaotoa ukomo wa bajeti waweze kuliona kwa macho ya kipekee” amesisitiza Mhe. Masanja.
Amesema kuna haja ya kufanya mabadiliko hasa katika mfumo wa uendeshaji wa chuo hicho kwa kuwafundisha vijana vitendo zaidi kuliko nadharia ili kuwawezesha kuchakata mazao ya misitu yenye ubora wa hali ya juu yatakayoweza kushindanishwa na bidhaa zinazotoka nje ya nchi.
Aidha, Ameilekeza Menejimenti hiyo kuzalisha vijana wakomavu na wenye taaluma ili wasaidie katika uhifadhi wa misitu kutokana na nchi kukumbwa na changamoto ya uvamizi wa misitu na ukataji wa miti hovyo.
Amesema Wizara ya Maliasili na Utalii ina matumaini makubwa na vijana wanaopatiwa ujuzi katika chuo hicho na kwamba wanakwemda kuwa Mabalozi wa kuielimisha jamii kuhusu umuhimu wa kutunza misitu sambamba na kuongeza mnyororo wa thamani wa mazao ya misitu
Katika hatua nyingine, Mhe. Masanja amesema Wizara itaendelea kutatua changamoto zinazokikaboli chuo hicho ikiwa ni pamoja na kuongeza idadi ya watumishi na kuboresha muundo wa watumishi.
Awali, akiwasilisha taarifa ya utekelezaji Makamu Mkuu wa Chuo hicho , Stephen Kingwele amesema chuo kinakabiliwa na changamoto ya uhaba wa watumishi unaopelekea kuajiri watumishi wa mkataba ili kusaidia nguvukazi.Pia ameishukuru Wizara ya Maliasili na Utalii ambayo imekuwa ikisaidia fedha za utekelezaji wa majukumu kupitia Mfuko wa Misitu.
Naye, Mkuu wa Wilaya ya Arumeru , Mhe. Mhandisi Richard Ruyango amemshukuru Naibu Waziri kwa kufanya ziara katika chuo hicho kwa kuwa ndio mwanzo wa kutatuliwa kwa changamoto mbalimbali zinazokikabili.
Chuo cha Misitu Olmotonyi kilianzishwa mwaka 1937 kwa lengo la kuzalisha wafanyakazi katika sekta ya misitu ili kuwepo na uhifadhi endelevu.