Ndugu Wanahabari,
Kama mnavyofahamu, Sheria ya Benki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006, imeipa Benki Kuu ya Tanzania mamlaka ya kusimamia shughuli zote za kibenki na taasisi za fedha nchini kwa lengo la kuhakikisha uimara na ustahimilivu wa sekta ya benki na ya fedha kwa ujumla.
Napenda kuwataarifu kuwa, kwa mamlaka iliyopewa chini ya kifungu namba 56(1)(g)(i) &(iii) cha Sheria ya Benki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006, Benki Kuu ya Tanzania imeiweka Yetu Microfinance Bank Plc chini ya usimamizi wake kuanzia leo, Jumatatu, tarehe 12 Disemba, 2022.
Uamuzi huu umechukuliwa kutokana na Yetu Microfinance Bank Plc kuwa na upungufu mkubwa wa ukwasi na mtaji kinyume na matakwa ya Sheria ya Benki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006 na kanuni zake. Upungufu huu wa ukwasi na mtaji unahatarisha usalama wa sekta ya fedha. Pia, Yetu Microfinance Bank Plc kuendelea kutoa huduma za kibenki, kutahatarisha usalama wa amana za wateja wake.
Ndugu Wanahabari,
Kutokana na uamuzi huo, Benki Kuu ya Tanzania imeisimamisha Bodi ya Wakurugenzi na Uongozi wa Yetu Microfinance Bank Plc kuanzia leo tarehe 12 Disemba, 2022. Aidha, Benki Kuu ya Tanzania imemteua Meneja Msimamizi ambaye atakuwa na jukumu la kusimamia shughuli za Yetu Microfinance Bank Plc kwa kipindi ambacho itakuwa chini ya usimamizi wa Benki Kuu ya Tanzania. Umma unaarifiwa kuwa katika kipindi kisichozidi siku tisini (90) kuanzia siku ya taarifa hii, shughuli za utoaji wa huduma za kibenki za Yetu Microfinance Bank Plc zitasimama ili kuipa nafasi Benki Kuu kutathmini hatua za kuchukua ili kupata ufumbuzi wa suala hili.
Benki Kuu inapenda kuuhakikishia umma kuwa itaendelea kulinda maslahi ya wenye amana katika mabenki kwa lengo la kuleta ustahimilivu katika sekta ya fedha.
BENKI KUU YA TANZANIA
12 Desemba 2022