Home LOCAL WAZIRI UMMY AUNDA KAMATI KUCHUNGUZA MRADI WA UJENZI WA HOSPITALI YA RUFAA...

WAZIRI UMMY AUNDA KAMATI KUCHUNGUZA MRADI WA UJENZI WA HOSPITALI YA RUFAA UKEREWE.

Na:  WAF – Ukerewe, Mwanza

Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu ameunda timu ya Watu watano itakayoongozwa na Jaji Mstaafu Thomas Mihayo kufanya uchunguzi wa utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Ukerewe kufuatia malalamiko ya uwepo wa ubadhirifu wa fedha kwenye mradi huo.
 
Waziri Ummy amebainisha hayo leo Jumatano Disemba 21, 2022 wakati wa ziara yake Wilayani Ukerewe alipofika kukagua mwenendo wa ujenzi wa mradi huo kufuatia agizo la Mhe. Makamu wa Rais alipofanya ziara yake wilayani humo Novemba 25, 2022 na kumtaka Waziri wa Afya kufika kukagua mwenendo wa ujenzi kutokana na malalamiko ya wananchi.
 
“Niseme wazi, kwa macho mimi nimeona kuwa gharama za ujenzi kwenye mradi huu zipo juu na haziendani kabisa na thamani ya fedha zilizolipwa hakuna Bilioni 2.6 pale, hivyo naunda timu yangu ambayo itaongozwa na Jaji Mstaafu Thomas Mihayo ambayo itachunguza malalamiko ya wananchi wa Ukerewe kwenye mradi wao”,’ amesema Waziri Ummy.
 
Amefafanua kuwa ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Ukerewe uliasisiwa na Waziri Mkuu Mhe Kassim Majaliwa alipofika Wilayani humo na kubaini uhitaji wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ili wananchi wa Ukerewe wasisafiri tena kwenda Jijini Mwanza katika Hospitali ya Sekou Toure au Bugando lakini watekelezaji wameamua kuiboresha Hospitali ya Wilaya badala ya kujenga hospitali mpya ambayo ingejumuisha huduma za kibingwa za matibabu zinazoendana na miundombinu.
 
“Hamjanishawishi kuwa baada ya Ujenzi huu wanaukerewe watapata huduma za kibingwa hapa hivyo hatujatatua tatizo maana huduma zinazotolewa hapa bado zipo kwenye Hospitali ya Wilaya ambayo inatumika na mwanamke ambaye atafika hapa na matatizo makubwa ya uzazi bado hatosaidiwa hivyo ni lazima tutafakari hilo na tujielekeze huko.” Mhe. Waziri amefafanua.
 
Waziri Ummy amebainisha kuwa Kamati hiyo aliyounda ni yake hivyo itachunguza ujenzi wa majengo yaliyojengwa kwa gharama za Shilingi Bilioni 2.6 huku wajumbe wengine wa Kamati hiyo watakakuwa ni Wawakilishi wawili kutoka Bodi ya Wasajili Wahandisi, Mhakiki Majengo kutoka Ofisi ya Kanda ya Ziwa, Mwakilishi kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali huku akionyesha kusita kumuweka Mwakilishi wa Wizara kutokana na  Wizara kutuhumiwa katika ucheleweshaji wa mradi huo.
 
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Adam Malima amesema kuwa kumekua na makosa tangia hatua za awali katika utekelezaji wa ujenzi wa mradi huo kwa kutofuata taratibu za malipo, kutekelezwa kwa kuchelewa na miundombinu kutozingatia mahitaji halisi ya wananchi kwenye huduma za kibingwa.
 
Naye Mbunge wa Jimbo la Ukerewe Mhe. Joseph Mkundi amesema kwenye utekelezaji wa mradi huo wananchi wa Ukerewe wanakwazwa na mpango wa Miundombinu ya majengo, ucheleweshaji wa Ujenzi huo na thamani ya mradi kuonekana kuwa chini ya fedha zilizolipwa kwa Mkandarasi na ametoa wito kwa Wizara kusaidia kupata suluhu ya jambo hilo ili mradi ukamilike.
 
“Katika wilaya yetu ya Ukerewe tuna visiwa 38 wananchi na wanawake wenzangu kwenye visiwa hivyo wanapata shida sana ya huduma za uzazi, nikuombe tupate vituo vya afya kwenye visiwa vikubwa ili wananchi walio wengi wapate huduma za Afya bila kusafiri umbali mrefu kuja kwenye Hospitali ya wilaya.” Mhe. Furaha Matondo, Mbunge viti Maalum.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here