Home BUSINESS VITUO ATAMIZI KUWA KICHOCHEO CHA MABADILIKO SEKTA YA MIFUGO NCHINI

VITUO ATAMIZI KUWA KICHOCHEO CHA MABADILIKO SEKTA YA MIFUGO NCHINI

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki, akizungumza na washiriki wa MafunzoRejea ya Maafisa Ugani wa Kanda ya Mashariki wakati akifungua mafunzo hayo yaliyofanyika mkoani Pwani jana Desemba 13, 2022. 

Na: Mbaraka Kambona, Pwani 

WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki amesema kuwa Wizara yake imeanzisha vituo atamizi kuwawezesha vijana kufuga kwa tija ili kujikwamua kimaisha na pia kuwa ni kichocheo kwa wafugaji wengine kujifunza kwa vitendo na kubadilika kutoka katika ufugaji wa kienyeji na kufanya ufugaji wa kisasa utakaowaletea tija zaidi na kupunguza migogoro isiyo ya lazima kati ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi.

Ndaki aliyasema hayo wakati akifunga Mafunzo Rejea kwa Maafisa Ugani wa Kanda ya Mashariki yaliyofanyika mkoani Pwani jana Desemba 13, 2022.

Alisema kuwa Wizara yake imewekeza na inahamasisha Vijana kushiriki katika uzalishaji wa mifugo kupitia Vituo Atamizi ambapo kwa mwaka wa fedha 2022/2023 vijana 240 waliohitimu vyuo vya Mafunzo ya Mifugo wamedahiliwa na kuanza mafunzo ya unenepeshaji wa ng’ombe katika vituo nane (8).

“Kwa mantiki hiyo nawahimiza wadau mbalimbali kuwekeza na kuhamasisha vijana kujiunga na Vituo atamizi ambavyo vimeanzishwa na Wizara kwa sababu vijana hao wakimaliza mafunzo hayo watasaidia wafugaji wengine kubadilika na kuanza kufuga kwa tija,” alisema Ndaki.

“Mwakani tunatarajia kuwa na vijana wengi zaidi kwa sababu tutaongeza bajeti kuhusu vituo hivi ili tuweze kuwachukua vijana wengi zaidi hata kufikia 1000, kwa sababu vijana hawa wakitawanyika kote nchini wataleta mageuzi kwenye ufugaji wetu,”alifafanua 

Aidha, alisema kuwa huduma za ugani ni kiungo muhimu kati ya watafiti na wafugaji ili kupata ufugaji wenye tija hivyo ni vyema maafisa ugani wakaimarisha mahusiano mazuri ili waweze kufikia malengo tarajiwa.

“Nitoe rai kwenu kujenga ushirikiano madhubuti baina yenu na wafugaji utakaowezesha kutoa taarifa sahihi, kusambaza teknolojia, kuelimisha, kutoa ushauri wa kitaalamu na kupata mrejesho,”alisema.

Waziri Ndaki alisema kuwa wanatambua  changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya mifugo hususan katika utoaji wa huduma za Ugani hapa nchini lakini tayari Wizara kupitia Mpango wa Mabadiliko wa Sekta ya Mifugo imebainisha mikakati na afua mbalimbali za kuzipatia suluhisho changamoto hizo.

“Miongoni mwa juhudi za serikali ni pamoja na kuanza kutoa Mafunzo Rejea kwa Maafisa Ugani Watakaowafundisha Wengine (Trainer of Trainee) ambapo jumla ya Maafisa Ugani 800 watafikiwa kwa mwaka wa fedha, 2022/2023. Aidha, Wizara inatarajia kutoa mafunzo elekezi kwa wafugaji 182,200 nchini ambapo ninyi mtatusaidia sana katika kutekeleza jukumu hilo,”alifafanua.

Aliongeza kuwa katika kutatua changamoto ya ukosefu wa vitendea kazi vya
kutolea huduma za Ugani, Wizara imepanga kununua pikipiki 1,200 ambazo zitaongeza
chachu kama vitendea kazi muhimu katika Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka ya
Serikali za Mitaa. Vilevile Wizara imeanza matumizi ya mifumo ya TEHAMA
(M-Kilimo na Digital Agricultural Service Portfolio (Ugani Kiganjani) kwa lengo
la kuwafikia wafugaji wengi na kutoa mrejesho wa kila kazi ambayo Afisa Ugani
atakuwa ametekeleza katika eneo lake.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki(kulia) akiongea na Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani, Bi. Zuwena Omary alipotembelea Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani muda mfupi kabla ya kwenda kufunga Mafunzo Rejea ya Maafisa Ugani Kanda ya Mashariki yaliyofanyika mkoani Pwani Disemba 13, 2022.

Washiriki wa mafunzo hayo wakifuatilia hutuba ya ufunguzi wakati ikiwasirishwa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (katikati) akimsikiliza Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti, Mafunzo na Huduma za Ugani, Dkt. Angello Mwilawa (kulia) wakati akiagana na Mkurugenzi huyo punde baada ya kufunga Mafunzo Rejea ya Maafisa Ugani Kanda ya Mashariki yaliyofanyika mkoani Pwani Disemba 13, 2022. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Mhe. Sara Msafiri.

Previous articleWAZIRI MKUU AWATAKA WATUMISHI MLELE WAHAMIE KWENYE NYUMBA ZA SERIKALI
Next articleWAKUU WA MIKOA HAKIKISHENI MBOLEA INAWAFIKIA WAKULIMA-MAJALIWA
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here