Home BUSINESS TPDC YAENDESHA ZOEZI LA UTOAJI ELIMU YA MANUFAA, ULINZI NA USALAMA WA...

TPDC YAENDESHA ZOEZI LA UTOAJI ELIMU YA MANUFAA, ULINZI NA USALAMA WA MIUNDOMBINU YA GESI ASILIA KWA VIJIJI VYA MKOA WA LINDI

Baadhi ya wananchi wakisikiliza mada kutoka kwa Afisa Maendeleo ya Jamii wa TPDC Bw. Oscar Mwakasege wakati wa zoezi la utaoji elimu kwa umma
 
**
 
Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limeendesha zoezi la utoaji elimu kwa vijij na mitaa inayoguswa na miundombinu ya gesi asilia, TPDC imekua na utaratibu wa kutoa elimu kwa umma juu ya miradi mbalimbali ya utafiti na uendelezaji wa nishati ya mafuta na gesi asilia nchini.

 Elimu hii inatolewa ikiwa ni sehemu ya kuimarisha mahusiano mazuri kati ya TPDC na wadau wake, kuwajengea uwezo wananchi kutambua fursa zinazoambatana na uwekezaji wa miradi ya gesi pamoja na kuimarisha ulinzi na usalama wa miundommbinu ya miradi ikiwemo miundombinu ya bomba la gesi asilia .
 
Zoezi la utoaji elimu kwa mkoa wa Lindi limefanyika kupitia mikutano ya hadhar katika vijiji ambavyo vimeguswa na mradi wa bomba la gesi asili ambapo elimu hiyo ilijikita kwenye mada za ulinzi na usalama, fursa zinazoambatana na miradi ya gesi asilia (manufaa) pamoja na Uwajibikaji wa Shirika kwa jamii (CSR).
 
 Akiongea katika moja ya mikutano na wananchi wa Somanga Kusini, Afisa Maendeleo ya jamii wa TPDC Oscar Mwakasege ameeleza kuwa utunzaji na usalama wa mradi wa bomba la gesi asilia nchini ni pamoja na ushirikishwaji wa wananchi katika ngazi zote hususani katika kupata taarifa, elimu, utekelezaji wa miradi ya kijamii pamoja na ushirikishwaji kwenye ulinzi na usalama.
Baadhi ya wananchi wa kijiji cha Mavuji wakisikiliza na kuchangia mada katika zoezi la utoaji elimu lililoendeshwa na TPDC.
 
 
Aidha, katika kuelezea faida za mradi Bw. Mwakasege aliendelea kwa kusema kuwa mradi wa bomba la gesi asili umekua na manufaa makubwa kwa jamii na taifa kwa ujumla ambapo hadi sasa asilimia 70% ya umeme nchini unazalishwa kwa kutumia gesi asilia hivyo kuchagiza ukuaji wa sekta mbalimbali, matumizi kwa viwanda mbalimbali ambapo takribani viwanda 53 nchini vinatumia nishati ya gesi asilia, uendeshaji wa magari makubwa na madogo-zaidi ya magari 1500 yanatumia gesi asilia, matumizi ya kupikia majumbani ambapo mradi huu umetekelezwa Dar es salaam, Mtwara na Lindi (Mnazi mmoja).
 
 Vilevile Mwakasege aliongeza na kusema kuwa kila Halmashauri ambayo imeguswa na mradi wa bomba la gesi asilia inapokea sehemu ya fedha za mauzo ya gesi asilia kama mrabaha . Pia, tangu kuanza kwa matumizi ya gesi asilia Taifa limeokoa kiasi cha Tsh Trilioni 40 ikiwa ni mbadala wa matumizi ya mafuta.
 
Katika hatua nyingine Kaimu Mkuu wa kitengo cha usalama TPDC Fredy Mfikwa alieleza kuwa mradi wa bomba la gesi asilia umegusa vijiji na mitaa 139 kuanzia Msimbati Mtwara hadi Dar es salaam. Aidha, alieleza kuwa TPDC inashirikiana vizuri na vijiji/mitaa hiyo kwenye suala la ulinzi na usalama ikiwa ni pamoja na kutoa fedha kila mwezi kwa kila kijiji/mtaa ili kuwezesha vijiji hivyo kufanya usafi kwenye njia (Mkuza) wa bomba la gesi asilia.
 
Bw.Mfikwa aliendelea kwa kutoa rai kwa wananchi kuendelea kuitunza miundombinu ya bomba la gesi asilia kwa kukomesha shughuli hatarishi za kibinadamu ndani ya miundiombinu ya bomba la gesi asilia, pamoja na kuwasisitiza wananchi kuendelea kutoa taarifa kwa uongozi wa viijiji/mtaa au TPDC pindi wanapoona mazingira hatarishi ndani ya miundombinu ya bomba la gesi asilia.
 
“Shughuli za kibinadamu ndani ya Mkuza wa bomba la gesi asilia kama kuchimba mchanga, kilimo cha mazao ya muda mfupi na mrefu, kuchoma nyasi moto, kupitisha makundi makubwa ya mifugo na shughuli zozote za ujenzi haiziruhusiwi, hivyo natoa rai kwa uongozi wa vijiji na wananchi kuendelea kudumisha ulinzi na usalama ili bomba hili liendelee kuwa na manufaa kwa sasa na baadae’’ alieleza Mfikwa.
Kaimu Mkuu Kitengo cha usalama TPDC akitoa elimu ya ulinzi na usalama wa miundiombinu ya gesi asilia.
 
 
Kwa upande mwingine akielezea Uwajibikaji wa Shirika kwa Jamii (CSR) Afisa Maendeleo ya Jamii Kwigema Anthony alisema kuwa Uwajibikaji kwa jamii ni kipaumbele cha TPDC kwani hadi sasa zaidi ya bilioni 1.5 zimetumika kutekeleza miradi mbalimbali ya kuinua huduma za kijamii kwenye maeneo ambayo TPDC inatekeleza miradi yake. 
 
Aidha kwa mkoa wa Lindi TPDC imetekeleza ujenzi wa miradi ya maji vijijini mfano mradi wa maji katika kijiji cha Songosongo na Kilangala B, ujenzi wa vyoo mashuleni, ujenzi wa madarasa, ujenzi wa majengo ya maabara mashuleni, kudhamini michezo pamoja na ujenzi wa majengo ya ofisi za serikali za mitaa na vijiji.
 
 
Sambamba na zoezi la utoaji elimu kwa jamii, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) lilikabidhi Viti na Meza 85 katika Shule ya Sekondari Kikanda iliyopo Kata ya Tingi Wilaya ya Kilwa ikiwa ni sehemu ya Uwajibikaji wa Shirika kwa Jamii, akiongea katika hafla ya kukabidhi samani hizo Afisa Maendeleo ya Jamii wa TPDC Kwigema Anthony alisema kilichofanyika ni muendelezo wa TPDC kuunga mkono juhudi za serikali katika kuinua huduma za elimu nchini.
 
 
Wakitoa shukrani zao baadhi ya wanafunzi, walimu na viongozi wa kata wamepongeza TPDC kwa kuwapatia samani tajwa na kueleza kuwa samani hizo vitawasaidia wanafunzi kujifunza kwa ufanisi mkubwa kwani hakutakua na mbanano ambao ulikuwepo awali.
Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Kikanda wakipokea viti na meza kutoka TPDC.
Previous articleWAZAZI WAASWA KUWEKA MSUKUMO WA KUTOA ELIMU YA AFYA YA UZAZI KWA VIJANA   SHULENI KUEPUSHA MIMBA ZA UTOTONI
Next articleSERIKALI INAFANYA MABORESHO MAKUBWA MUHIMBILI-MAJALIWA
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here