Home LOCAL TANESCO WAPAMBANA KUMALIZA UPUNGUFU WA UMEME, WAONGEZA MEGAWATTS 135

TANESCO WAPAMBANA KUMALIZA UPUNGUFU WA UMEME, WAONGEZA MEGAWATTS 135

Na Beatrice Sanga -MAELEZO- Decemba 02, 2022

Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Linaendelea kufanya jitihada za muda mfupi na za muda wa kati katika kukabiliana na tatizo la upungufu wa umeme ikiwemo kukamilisha matengezo ya mtambo mmoja wa LM6000 katika kituo cha ubungo namba III, ambao umeshaanza kuingiza megawati 35 za umeme katika Gridi ya Taifa hali inayopelekea kiasi cha upungufu wa umeme kupungua.

Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam leo Desemba 02, 2022, Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, Maharage Chande amesema pamoja na mtambo huo, mitambo mingine miwili imetengenezwa na kukamilika kwa wakati ukiwepo mtambo wa kituo cha Kidatu pamoja na kituo cha Kinyerezi namba II.

“Kama nilivyosema mtambo wetu wa Kidatu haujafanyiwa matengenezo kwa muda mrefu lakini tuliahidi kuwa Tarehe 30 matengenezo yafanyike na mtambo huo urudi, mpaka sasa tunavyoongea matengenezo yamefanyika na Leo unazalisha mpaka megawati 40 mpaka asubuhi kufikia hii, pia tulisema kituo cha Kinyerezi tutahakikisha tunapata megawati 60 tayari umeshaanza kuzalisha megawati 215 za umeme kuanzia tarehe Novemba 2022” Amesema Bw. Chande.

Bw. Chande amesema kuwa mpaka kufikia Novemba 23, kulikuwa na upungufu wa umeme kati ya megawati 300 hadi 350 lakini mpaka leo upungufu umeshuka mpaka megawati 200 hadi 220, hali inayoonyesha juhudi za kupunguza upungufu wa umeme zinazaa matunda lakini pia TANESCO itaendelea kuchukua juhudi mbalimbali za muda mfupi na muda wa kati ili kutatua kabisa matatizo ya umeme.

Aidha amesema iwapo mvua zitaendelea kunyesha katika mabwawa yote ya kufua umeme na matengenezo yaliyobakia kukamilika kama yalivyopangwa, hali ya umeme itaendelea kuimarika na kiasi cha upungufu wa umeme kuendelea kupungua kutoka wastani wa kati ya megawati 300 hadi 350 wiki iliyopita hadi kufikia megawati 215 za umeme wiki hii.

MWISHO

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here