Home LOCAL REA YAZINDUA MRADI WA KUSAMBAZA UMEME MAENEO YA VIJIJI MIJI SINGIDA, MKANDARASI...

REA YAZINDUA MRADI WA KUSAMBAZA UMEME MAENEO YA VIJIJI MIJI SINGIDA, MKANDARASI AKABIDHIWA RASMI MBELE YA DC

Mkuu wa Wilaya ya Singida Mhandisi Paskas Muragili (katikati) kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Singida akiwasha kifaa maalumu cha kupiga king’ora kuashiria uzinduzi rasmi wa mradi mpya wa kusambaza umeme kwenye Vijiji Miji viliyopo pembezoni mwa Manispaa ya Singida katika hafla iliyofanyika Kata ya Mwankoko Desemba 29,2022 ambao utagharimu Sh. 7.11 Bilioni zilizotolewa na Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) amapo  Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) litakuwa msimamizi wa mradi huo. 

Na: Dotto Mwaibale, Singida

SERIKALI kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imezindua mradi mpya wa kusambaza umeme kwenye Vijiji Miji viliyopo pembezoni mwa Manispaa ya Singida ambao utagharimu Sh. 7.11 Bilioni na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) litakuwa msimamizi wa mradi huo.

Mradi huo wa kusambaza umeme katika Vijiji Miji (Peri-urban Electrification)  ambao umezinduliwa Desemba 29, 2022 Kitongoji cha Kitope Darajani Kata ya Mwankoko utatekelezwa kwenye vitongoji 34 vilivyopo katika  Kata 9 ambapo wateja watarajiwa
ni zaidi ya 2000.

Akizindua Mradi huo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mkuu wa Wilaya ya Singida Mhandisi Paskas Muragili aliwaomba wananchi wachangamkie mradi huo kwa kuanza kusuka  nyaya za umeme katika nyumba zao ili waweze kufungukiwa kwa gharama ya Sh.27,000.

“Mradi huu ukikamilika unakwenda kubadilisha uchumi wa wanananchi kwani watautumia umeme huo kuanzisha viwanda vidogo  na shughuli zingine za uzalishaji ambazo zitatumia nishati hiyo hivyo kuinua uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla” alisema Muragili.

Muragili alimuomba mkandarasi wa mradi huo kuukamilisha ndani ya mwaka mmoja badala ya miezi 18 aliyopewa  kuukamilisha kwa sababu hakuna sababu yoyote ya kuchelewa kuukamilisha ndani ya muda huo kwa kuwa unatekelezwa kwenye maeneo yenye miundombinu mizuri ya barabara.

Akifafanua kuhusu Mradi huo, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Nicolaus Moshi  alisema mradi wa usambazaji nishati ya umeme katika maeneo yaliyo pembezoni mwa miji kwa hapa nchini Mkoa wa Singida ndio wanaupata kwa mara ya kwanza.

Alisema mradi huo utajenga jumla ya kilomita 40.5 za msongo wa kati na msongo mdogo na kupitia mradi huo watafunga mashine umba au Transfomer 33 katika vitongoji vilivyotajwa na kuweza kuwaunganishia wateja wa awali 1802 ambapo aliwaomba wananchi wa maeneo utakapo pita mradi huo kuchangamkia fursa hiyo.

Moshi alisema REA imekuwa ikitekeleza miradi mingine mingi hapa nchini Mkoa wa Singida ukiwa ni moja ya mikoa ambayo inanufaika na miradi hiyo na akatumia
nafasi hiyo kumtambulisha kwa wananchi na mgeni rasmi Mkandarasi wa Kampuni ya  Central Electricals International Ltd anayetekeleza mradi huo na kukabidhiwa rasmi mbele ya mgeni rasmi Mkuu wa Wilaya ya Singida, Mhandisi Paskas Muragili ili aanze kufanya kazi .

Katika hafla hiyo viongozi mbalimbali walipata fursa ya kutoa salamu huku wakimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za kutekeleza mradi huo na mingine mingi na wito wao mkubwa wakiomba wananchi kutunza miundombinu ya mradi huo na kuwataka wachangamkie umeme huo kwa kuanzisha miradi ya kuinua uchumi wao.

Previous articlePELE AFARIKI DUNIA
Next articleWAZIRI JAFO AWATAKA WANANCHI KUTUNZA MIRADI
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here