Home Uncategorized RAIS SAMIA KUKUTANA NA WADAU WA HABARI JIJINI DAR

RAIS SAMIA KUKUTANA NA WADAU WA HABARI JIJINI DAR

ZAIDI ya wanahabari na wadau wa habari 1000 nchini, watakutana na kuzungumza na Rais Samia Suluhu Hassan tarehe 17 Desemba 2022, jijini Dar es Salaam.

Akizungumzia mkutano huo tarehe 5 Desemba 2022, Deodatus Balile, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), alisema mkutano huo utafanyika ikiwa ni wito wa Rais Samia alioutoa tarehe 3 Mei 2022, katika Kilele cha Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani, jijini Arusha.

“Mheshimiwa Rais Samia atakutana na waandishi wa habari tarehe 17 mwezi huu, na imepangwa angalau kuhudhuriwe na wanahabari 1000.

“Utakumbuka mwezi Mei, Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani, Arusha alisema, tumuandalie mkutano ili akutane na wanahabari wa ndani,” alisema Balile.

Balile alisema, mkutano huo unafanyika baada ya wadau wa habari kukutana na serikali katika hatua mbalimbazi za kupitia vifungu vya sheria ya habari vinavyonekana kukandamiza tasnia hiyo.

Na kwamba, mkutano wa wanahabari na Rais Sami ani fursa nyingine kwa tasnia ya habari nchini kuelekea safari ya mabadiliko ya sheria ya habari.

“Baada ya kufanya vikao na Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, sasa ni wakati wa kufika mbele ya Rais Samia kwa ajili ya kueleza hatua mbalimbali zilizofikiwa.

“Katika mchakato huu, tumekuwa tukishiriki kuzungumza na Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ili tukubaliane katika sehemu mbalimbali ya vifungu vya sheria ya habari,” alisema Balile na kuongeza:

“Tulifanya mkutano wa mwisho mwezi Novemba ambao tulisema, sasa huu uwe mkutano wa mwisho ili sheria ya huduma za habari ipelekwe bungeni.”

Akizungumzia mchakato wa vikao vya serikali na wadau wa habari, Balile alisema serikali ilipeleka mawazo yake kwenye vikao hivyo na kwamba, hatua iliyofikiwa imeridhiwa na wadau wa habari nchini.

“Serikali ilikuja na mawazo mengi mazuri na tukaona kwamba sasa twende mbele ya mheshimiwa rais, tueleze tulikofikia.

“Kutakuwepo mada mbalimbali ambapo zitawasilishwa halafu tutakuwa na majumuisho, lakini kikubwa tunaangalia maendeleo ya nchi yetu katika miaka 61 ya Uhuru, kwamba tulikuwa wapi na sasa tuko wapi,” alisema Balile.

Mwenyekiti huyo wa TEF alisema, kwa kufanya hivyo, mchango vya vyombo vya habari kuanzia uhuru utaonekana wazi katika dhana nzima ya Uhuru.

“Wazee wetu walipigania Uhuru wa kisiasa, sasa vyombo vya habari vianze kutengeneza ajenda ya uhuru wa kiuchumi kwamba, wananchi waanze kuzungumzia maeneo ulipo uchumi.

“Baada ya Uhuru vyombo vya habari vijielekeze katika shughuli za biashara, na pale sheria zinapokua ngumu, tuanze kuzungumza tutakavyorekebisha. Iwe ajenda na serikali ifanye kazi ya kuwezesha sekta binafsi na taasisi mbalimbali za watu binafsi na hata serikali yenyewe kurahisisha utendaji wa shughuli za biashara,” alisema.

Balile alisema, pamoja na mambo mengine, kwenye mkutano huo itaelezwa miaka 61 iliyopita tulikuwa wapi na sasa tupo wapi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here