Home LOCAL NAIBU WAZIRI MASANJA ASHAURI MFUMO WA AJIRA ZA WALIMU UBORESHWE KUKABILIANA NA...

NAIBU WAZIRI MASANJA ASHAURI MFUMO WA AJIRA ZA WALIMU UBORESHWE KUKABILIANA NA UHABA WA WALIMU VIJIJINI

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) ametoa mapendekezo ya kuboreshwa kwa mfumo wa ajira za walimu wa shule za msingi na sekondari ili kukabiliana na changamoto ya uhaba wa walimu katika maeneo ya vijijini.

Ameyasema hayo wakati wa kikao cha Kamati ya Ushauri cha Mkoa wa Mwanza kilichofanyika leo katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mwanza ambapo pamoja na mambo mengine kilijadili namna ya kukabiliana na upungufu wa walimu vijijini.

Amesema ili kuwafanya walimu kubaki katika vituo vya kazi bila kuhama , ni vyema ajira zinapotoka kipaumbele kiwe kwa wale walio tayari kufanya kazi vijijini.

Amesema uwekwe utaratibu kila anayeomba ajira ya ualimu aingie mkataba na Serikali kwamba kwa miaka kumi atakaa katika kituo cha kazi bila kuhama na kuweka bayana kuwa hii itapunguza uhaba wa walimu vijijini.

Katika hatua nyingine, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza ,Mhe. Adam Malima amesema ili kuboresha elimu mashuleni ni lazima kuweka utaratibu wa kufanya kwa wazazi wanaowakingia vifua wanaume wanaowapa mimba wanafunzi.

“Ni lazima tushughulike na wazazi hawa pamoja na watu wazima wasiojiheshimu wanaowaharibu wanafunzi wakiwa masomoni” amesisitiza.

Kikao hicho kimehudhuriwa na Wabunge wa Mkoa wa Mwanza, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri za Jiji la Mwanza , Wakuu wa Taasisi mbalimbali za Serikali na watoa huduma mbalimbali za kijamii.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here