Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mwanza, ambaye pia ni Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja akiwa ameambatana na Umoja wa Wanawake wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Magu amegawa vifaa tiba vyenye thamani ya shilingi milioni 14 kwa Hospitali ya Wilaya ya Magu pamoja na mitungi ya gesi 100 kwa wanawake wajawazito.
Akizungumza leo katika hafla ya ugawaji wa vifaa hivyo vyenye thamani ya shilingi 14,575,000 na mitungi ya gesi 100 kwenye Hospitali ya Magu, Mhe. Masanja amesema vifaa hivyo vimetokana na mchango wake binafsi pamoja na mchango wa Doris Mollel Foundation.
Amefafanua kuwa vifaa tiba hivyo vitasaidia kuokoa maisha ya watoto waliozaliwa njiti na pia mitungi ya gesi itasaidia wanawake wajawazito kupunguza shughuli nzito za kutafuta nishati mbadala.
Mhe. Masanja amewaasa wanawake wajawazito kuhudhuria kliniki mara kwa mara ili kujua maendeleo ya mtoto anapokuwa tumboni.
Aidha, Mhe. Masanja amewataka wanawake wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada anazozifanya za kuwaletea maendeleo wananchi wa Tanzania.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Wilaya ya Magu Dkt.Maria Kapinga amesema vifaa hivyo vilivyotolewa na Naibu Waziri Masanja vitasaidia kunusuru maisha ya watoto wanaozaliwa kabla ya muda ( njiti).