Na Maiko Luoga – Mwanza
Kanisa Anglikana Tanzania limeiomba Serikali kupitia vyombo vya ulinzi na usalama mkoani Mwanza kuharakisha uchunguzi wa kifo cha Askofu mstaafu wa Dayosisi ya Victoria Nyanza DVN Boniface Kwangu aliyekutwa amefariki dunia na mwili wake kuokotwa katika ziwa Victoria karibu na Daraja la Magufuli Kigongo Feri Bukumbi Disemba 01, 2022.
Akizungumza kwenye Misa Takatifu ya mazishi ya Askofu Boniface Kwangu iliyofanyika Disemba 05, 2022 Kanisa Kuu Anglikana Mtakatifu Nikolas Jijini Mwanza, Askofu Mkuu wa Kanisa Anglikana Tanzania Maimbo Mndolwa amesema hadi sasa Kanisa halina taarifa rasmi ya chanzo cha kifo hicho.
“Tupo hapa kumsindikiza Baba Askofu Boniface Kwangu aliyefariki dunia na mwili wake kukutwa majini, tutumie nafasi hii kutoa pole kwa familia Mke na Watoto wa marehemu kwa msiba huu, tuviombe vyombo vyetu vya ulinzi na usalama kuhakikisha wanakamilisha mapema uchunguzi wa tukio hili ili tupate uhakika wa kifo cha Baba Askofu Boniface Kwangu” alieleza Askofu Maimbo Mndolwa.
Akitoa hotuba ya faraja kwa wafiwa na waombolezaji wa msiba huo Askofu wa Dayosisi ya Kagera Kanisa Anglikana Tanzania Darlington Bendankeha amewataka kuwa na uvumilivu kufuatia kifo cha Askofu Kwangu huku akitoa wito kwa jamii kuishi maisha ya hofu na kumpendeza Mungu kwakuwa kila Mwanadamu ataonja mauti.
“Tunaishi katika Dunia ambayo kimwili kila mtu anasema anampenda Yesu lakini aliyobeba moyoni anakijua mwenyewe Mungu aliyekupa uhai ipo siku atauchukua, Tuishi kwa hofu na kumtegemea yeye Tumpende kweli sio kinafiki na kuacha matendo mabaya” alieleza Askofu Darlington.
Baadhi ya Maaskofu wa Kanisa Anglikana, Makanisa ya CCT na waumini waliojitokeza katika Mazishi hayo wameeleza kusikitishwa na aina ya Kifo cha Askofu mstaafu Boniface Kwangu na kusema kama tukio hilo limefanywa na wanadamu linapaswa kukemewa kwa kila aina na hatua kali za kisheria zichukuliwe endapo muhusika au wahusika watapatikana.
Siku chache zilizopita Jeshi la Polisi Mkoani Mwanza lilitoa Taarifa za kupatikana mwili wa Askofu Kwangu ukielea majini na kusema kuwa wanaendelea na uchunguzi ili kubaini chanzo cha kifo hicho, hatua inayosubiriwa na waumini wa Kanisa Anglikana na Watanzania kwa ujumla.