Home LOCAL MAKALLA AMALIZA MGOGORO WA BARABARA KIGAMBONI

MAKALLA AMALIZA MGOGORO WA BARABARA KIGAMBONI

Na: Mwandishi wetu, DSM

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam Amos Makalla ameagiza barabara iliyokuwa ikileta mgogoro Kimbiji Manispaa ya Kigamboni baada mwekezaji kampuni ya ASM kujenga ukuta na kuifunga ifunguliwe.

Makalla jana alifanya ziara ya pili kwenye eneo hilo la mgogoro na kufanya kikao cha pamoja kati ya wawekezaji wa maeneo hayo, wananchi, viongozi na wataalam wa ardhi kutoka Manispaa ya Kigamboni pamoja na Wizara ya Ardhi.

Alisema, wameamua mwekezaji ASM alipwe fidia na ukuta huo ubomolewe ili barabara hiyo ya asili iendelee kutumika kama ilivyokuwa awali.

“Baada ya kupitia vielelezo vya ramani ya mipango miji toleo la mwaka 2021, tumeona hakuna uhalisia wa kuanzisha barabara mpya, tumeona barabara ni hii ya zamani inafaa, sasa nimeagiza leo hii huyu mwekezaji aandikiwe barua na imfikie leo hii kumtaarifu juu ya uwamuzi huu,” alisema Makalla.

Aidha, alisema kwa kuwa tathimini ya awali ya kumlipa fidia mwekezaji huyo ilishafanyika, mchakato huo uendele na ASM alipwe fidia ili barabara hiyo ianze kutumika.

“Gharama ya kuanzisha barabara mpya ambayo tumeonyeshwa hapa ni kubwa zaidi kuliko kumlipa fidia huyu mwekezaji, sasa maamuzi ya kikao tulichofanya ni hayo, utekelezaji wa kulipa fidia uanze mara moja, tumefanya hivi kwa manufaa mapana ya nchi” alisema Makalla.

Mgogoro huo wa ardhi umedumu kwa zaidia ya miaka saba ambapo umetokana na mwekezaji kampuni ya ASM (T) Ltd anayemiliki viwanja pacha vinavyotazamana kijiji cha Mikenge kata Kimbiji kuziba barabara inayoelekea kwenye fukwe ya bahari na kwa wawekezaji wengine.

Wananchi na wawekezaji wengine ambao walikosa barabara ya kupita walilalamika kwa Manispaa ya Kigamboni na kuomba barabara hiyo ifunguliwe.

Hata hivyo uongozi wa Manispaa ya Kigamboni kwa kushirikiana na mwekezaji ASM  walianzisha barabara nyingine iliyopita kando ya mto unaomwaga maji baharini kitendo ambacho wananchi na wawekezaji wengine walikipinga.

Akizungumza baada ya maamuzi hayo, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mikenge, Lameck Mayala, alisema uwamuzi huo ni wa busara na waliusubiri kwa muda mrefu.

“Kiukweli tunaishukuru sana Serikali kupitia kwa mkuu wetu wa Mkoa kwa maamuzi haya, hii barabara ilikuwepo kwa miaka mingi sana, ni barabara ambayo inawawezesha wananchi kufika baharini ambako wanafanya shughuri mbalimbali za kuwaingizia kipato, lakini pia wapo wawekezaji ambao walitoa ajira kwa vijana wetu kwenye hoteli zao walishindwa kufika kwenye maeneo yao, tunashukuru kwa maamuzi haya ya Serikali,” alisema Mayala.

Aidha, mmoja wa wawekezaji anayemiliki hoteli maeneo hayo ambaye biashara yake iliathirika kutokana na kufungwa barabara hiyo, Vidate Msoka, alisema maamuzi hayo yatawafanya kuendelea na biashara zao na kuchangia pato la taifa kwa kulipa Kodi.

“Biashara zetu zilisimama kwa muda, hatukuwa tunapata wateja kwa sababu ya kukosekana barabara ya kutufikisha hotelini, maamuzi haya yametupa faraja kubwa, tunashukuru” alisema Vidate.

Kwenye kikao hicho cha jana kilichokuwa chini ya Mkuu wa Mkoa Makalla, mwekezaji ASM hakuhudhuria licha ya kupewa taarifa na badala yake alitumia mwakilishi.

Licha ya juhudi za gazeti hili kumtafuta kwa njia ya simu kuelezea maamuzi yaliyochukukiwa haikupatikana.

Previous articleVIONGOZI WAANDAMIZI WA MAHAKAMA YA TANZANIA WAKUTANA NA WAHARIRI WA HABARI JIJINI DAR
Next articleJAFO AZINDUA JOSHO SIMANJIRO
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here