Na Mwandishi Wetu.
Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF),Deidatus Balile, amesema kuwa uhuru wa habari uliopo nchini hivi sasa, unapaswa kulindwa kisheria ili wanahabari waendelee kufanya kazi zao bila wasiwasi wowote.
Amesema kuwa wadau wa habari nchini wanafurahia uwepo wa uhuru huo lakini unapaswa kulindwa kisheria kwa serikali kufanya mabadiliko ya Habari.
“Wadau wa habari nchini wanafurahia uhuru wa habari uliopo nchini, tunaamini serikali italinda uhuru huu kisheria katika Mabadiliko ya Sheria ya Habari yajayo” amesena
Balile aliyasema hayo katika Kongamano la Kwanza la Maendeleo ya Sekta ya Habari tarehe 17 Disemba 2022 lililofanyika Jijini Dar es es Salaam ambapo alibainisha kuwa mabadiliko ya vipengele vya sheria ya habari. yatafikishwa bungeni Januari 2023.
“Nimezungumza na Waziri Nape (Nape Nnauye, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari) kuhusu mjadala wa Sheria ya Huduma za Habari, amesema Januari (2022) mapendekezo yatafikishwa bungeni,” amesema.
Akizungumzia madeni ya vyombo vya habari katika serikali na taasisi zake, Balile amesema licha ya juhudi kufanywa, bado taasisi za serikali ikiwemo halmashauri hasijalipa madeni yao kwa vyombo vya habari.
“Mpaka mwishoni mwa mwaka jana, madeni ambayo vyombo vya habari vinadai kwa serikali na taasisi zake ni Tsh. 7 bilioni.
“Ukijumuisha na deni la Gazeti la Daily News la serikali (Tsh. 11 Bilioni), jumla ya deni ni Tsh. 18 Bilioni na zaidi,” amesema.
“Halmashauri wana roho ngumu, hawajalipa mpaka leo licha ya kuandikiwa barua na TAMISEMI. Tunaomba mheshimiwa waziri (Nape) liwekee mguu chini, utusaidie,” amesema Balile.