Timu ya Dar es Salaam Young African (YANGA) imefanikiwa kufuzu hatua ya makundi ya Michuano ya Shirikisho Barani Afrika kwa kuibuka na ushindi wa goli 1-0 dhidi ya Club African ya nchini Tunisia.
Goli pekee la Yanga limefungwa na Mshambuliaji wake wa Kimataifa Stephanie Azizi Ki, katika dakika ya 78 ya mchezo huo kwa shuti Kali baada ya kuunganisha mpira wa kichwa aliopewa na Fiston Mayele.
Katika mchezo huo Yanga ilionesha mchezo mzuri kwa kucheza kwa nguvu ikilishambulia lango la mpinzani wake dakika zote.
Mchezo huo ni wa marudiano ambapo Mchezo wa kwanza ulipigwa katika Dimba la Mkapa Jijini Dar es Salaam na timu hizo kutoka Suluhu ya bila kufungana.