Home LOCAL WAZIRI MKUU ATOA AGIZO KWA WIZARA YA MAJI, DAWASA

WAZIRI MKUU ATOA AGIZO KWA WIZARA YA MAJI, DAWASA

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akifungulia maji kuyaruhusu kuingia katika tenki  lenye uwezo wa kuhifadhi lita milioni 70 za maji hayo. Hafla hiyo imefanyika Leo Novemba 2,2022 Kimbiji, Kigamboni Jijini Dar es Salaam 

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza na wananchi alipokuwa akitoa hotuba yake alipotembelea Mradi wa maji Kimbiji, Kigamboni Jijini Dar es Salaam 

Wananchi mbalimbali walioudhuria kwenye uzinduzi huo wakisikiliza hotuba ya Waziri Mkuu katika hafla hiyo.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam (mwenye shati nyeupe) akizungumza alipokuwa akitoa neno la shukrani muda mfupi baada ya zoezi la kufungulia maji.

Muonekano wa tenki la kuhifadhia maji lenye uwezo wa kuhifadhi lita milioni 70, ambalo Waziri Mkuu amelizindua leo.

( PICHA NA: HUGHES DUGILO)

*Ni kuhusu upatikanaji wa huduma ya maji Dar Es Salaam

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Maji kwa kushirikiana na sekta binafsi ihakikishe inakamilisha taratibu za utekelezaji wa mradi wa kutoa maji Mto Rufiji utakaosambaza maji katika maeneo ya mkoa wa Pwani na Dar es Salaam.

Pia, Mheshimiwa Majaliwa ameielekeza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar Es Salaam (DAWASA) iendelee kutenga fedha kwa ajili ya uchimbaji wa visima zaidi kwa ajili ya kuongeza uzalishaji wa maji. “Tusipokuwa makini tutaingia katika janga la ukame.”

Ametoa maagizo haya leo (Jumanne, Novemba 2, 2022) baada ya kukutana na Waziri wa Maji, Mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam, Muwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Pwani pamoja na viongozi wa DAWASA kwa ajili ya kujadili hali ya upatikanaji wa maji katika mkoa huo ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan.

Jana Novemba Mosi Mheshimiwa Rais Samia wakati wa Kongamano la Kitaifa la Nishati Safi ya Kupikia alimuagiza Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuhakikisha anasimamia uunganishwaji wa maji kutoka Kigamboni kuja maeneo mengine ya Jiji la Dar es Salaam pamoja na kuangalia maunganisho ya maji ili kukabiliana na uhaba wa maji katika Jiji hilo.

Waziri Mkuu amesema Serikali itahakikisha maeneo yote yanapata huduma za maji na kazi ya uchimbaji visima pamoja na kutafuta vyanzo vingine vya maji inaendelea ili kufikia matamanio ya Mheshimiwa Rais Samia ya kufikisha huduma ya maji karibu na makazi ya wananchi.

Akizungumza baada ya kukagua na kuwasha pampu ya maji katika mradi wa Visima vya Maji Kigamboni, Waziri Mkuu amesema visima hivyo ambavyo vinauwezo wa kuzalisha maji lita milioni 70 kwa siku vitasaidia katika kukabiliana na changamoto ya upungufu wa maji katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Dar Es Salaam.

Waziri Mkuu amesema mahitaji ya maji katika mkoa wa Dar Es Salaam ni lita 544 kwa siku na uzalishaji maji kwa siku ni lita 520 katika kipindi ambacho kiwango cha maji katika Mto Ruvu kinakuwa katika hali ya kawaida, hivyo kuwa na upungufu wa lita zaidi ya milioni 20.

“Katika kipindi hiki ambacho kiwango cha maji katika Mto Ruvu kimepungua uzalishaji wa maji nao umepungua na kufikia lita milioni 300 kwa siku, hivyo kusababisha upungufu wa lita milioni 244. Kwa sasa tukiingiza lita milioni 70 kutoka katika mradi huu wa visima vya Kigamboni tutakuwa na upungufu wa lita milioni 174, hivyo tutaupunguza changamoto ya upatikanaji wa maji katika baadi ya maeneo.”

Waziri Mkuu amesema katika mwaka wa fedha 2021/2022 Mheshimiwa Rais Samia alitoa shilingi bilioni 25 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa uchimbaji visima 10 katika eneo la Kigamboni, ambapo kati yake visima saba ndio vimewezesha upatikanaji wa lita milioni 70. Amewaagiza watendaji DAWASA waendelee na uchimbaji wa visima vingine.

Awali, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amesema katika kuhakikisha maji ya uhakika yanaendelea kupatikana katika maeneo mbalimbali nchini yakiwemo naya mkoa wa Dar Es Salaam, wizara inaendelea kufanya tathmini ya kutumia maji ya ardhini. Amesema kama wameweza kupata lita milioni 70 Kigamboni, hivyo anatarajia watapata maji mengi zaidi kupitia miradi ya uchimbaji wa visima.

Akizungumzia kuhusu mradi wa kutoa maji kutoka Mto Rufuji, Waziri huyo alisema wizara inaendelea na ufutialiji wa mradi huo ambao unatarajiwa kuzalisha maji lita milioni 750 kwa siku na hivyo kuondoa changamoto ya upatikanaji wa majisafi na salama katika maeneo ya mkoa wa Dar Es Salaam na Pwani.

 (mwisho)

IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU,

JUMANNE, NOVEMBA 2, 2022.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here