Watumishi wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), wametakiwa kuzingatia mafunzo ya maadili ya Utumishi wa Umma kwani yanawezesha watumishi kujisahisha pale wanapoteleza kimaadili.
Rai hiyo imetolewa na Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA Bw. Andrew Mkapa leo tarehe 26 Novemba, 2022 wakati akifungua Mafunzo ya Maadili ya watumishi katika Utumishi wa Umma, Kuzuia na Kupambana na Rushwa Mahala pa Kazi, katika ukumbi wa Chuo cha Utalii, jijini Dar es Salaam.
Bw. Mkapa amesema mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Taasisi ambao unahitaji kuelimishana kuhusu vita dhidi ya rushwa mahala pa kazi.
“Ni kawaida kwa binadamu kusahau, hivyo kuna uhitaji wa kukumbushana mara kwa mara ili tujisahishe pale tulipojisahau au kuteleza,” amefafanua Bw. Mkapa.
Akiwasilisha Mada kuhusu Maadili katika Utumishi wa Umma, Mwezeshaji kutoka Ofisi ya Rais Sekretarieti ya Maadili ya Utumishi wa Umma Bw. George Mwendamseke amesema msingi mkubwa wa maadili ya Utumishi wa Umma uko katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Pia amesema uwepo wa Sheria na kanuni mbalimbali pamoja na mifumo ya kimaadili lengo ni kukuza maadili na kufikia malengo ya kulinda ustawi wa wananchi.
“Watumishi mnapaswa kuhakikisha kuwa mnatoa huduma bora na zenye ufanisi kwa kuzingatia maadili ya kazi,” amesisitza Bw. Mwendamseke.
Bw. Mwendamseke amesema maadili mazuri ni kigezo cha ufanisi katika utendaji kazi kwani uwepo wake kunakuwa na uwajibikaji, kujituma na hatimaye kuleta tija kwa Taasisi
Bw. Mwendamseke amefafanua kuwa maadili ni pamoja na kujali muda, kutoa huduma bora, kuweka misingi ya haki bila upendeleo, kudumisha uhusiano mzuri mahala pa kazi, kujali wateja wa ndani na nje, kufanya kazi kama timu pamoja na mavazi.
Kwa upande wake mwezeshaji kutoka Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa (PCCB), Bw. Azina Mwisho amesema kuwa watumishi wa BRELA kupitia mafunzo hayo wanapaswa kujitathimini katika utendaji wao kazi kwani majukumu ya PCCB ni kuzuia na kupambana na rushwa hivyo elimu wanayoitoa ni kuzuia tabia za kuomba na kuchukua rushwa mahala pa kazi.
“Kwa kufuata Sheria, kanuni na taratibu, mtumishi unafanya majukumu yako kwa amani, bila woga wowote lakini unapokuwa na tabia za kuomba na kuchukua rushwa hutaweza kusimamia majukumu yako kiufasaha,” amefafanua Bw. Mwisho.
Mwezeshaji Bi. Neema Kilongozi kutoka PCCB kwa upande wake amewataka watumishi wa BRELA wanaume na wanawake kutotoa rushwa ya ngono mahala pa kazi kwani utendaji wao wa kazi unatokana na taaluma zao na si vinginevyo.
Amesisitiza kuwa mafunzo hayo ni chachu kwa watumishi kufanya yaliyo mema kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma.
Katika mafunzo hayo pia watumishi wamepata elimu kuhusu umuhimu wa Bima ya Maisha na elimu kwa kuwekeza kupitia kampuni ya Jubilee Life Insurance