Home LOCAL WATOA HUDUMA ZA AFYA ZAIDI YA 3,757 MKOA WA DAR ES SALAAM...

WATOA HUDUMA ZA AFYA ZAIDI YA 3,757 MKOA WA DAR ES SALAAM KUPATIWA MAFUNZO YA UTAYARI KUKABILIANA NA TISHIO LA EBOLA

Waziri wa Afya Mheshimiwa Ummy Mwalimu akisema jambo kwenye ufunguzi wa Kikao kazi cha mafunzo ya utayari wa kukabiliana na tishio la Ugonjwa wa Ebola kwa watoa huduma za afya 3,757 wa Mkoa wa Dar Es Salaam.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam Dkt. Rashid Mfaume akisema jambo kwenye Kikao kazi cha mafunzo ya utayari wa kukabiliana na tishio la Ugonjwa wa Ebola kwa watoa huduma za afya kwa Mkoa wa Dar Es Salaam.

Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Afya Duniani nchini Tanzania Dkt. Zabron Yoti akisema jambo kwenye Kikao kazi cha mafunzo ya utayari wa kukabiliana na tishio la Ugonjwa wa Ebola kwa watoa huduma za afya 3,757 wa Mkoa wa Dar Es Salaam.

.

 Na: Englibert Kayombo WAF- Dar Es Salaam

Serikali kwa kushirikiana na Shirika la Afya Duniani (WHO)wameanza kutoa mafunzo ya utayari wa kukabiliana na tishio la Ugonjwa wa Ebola kwa watoa Huduma za Afya zaidi ya 3,757 kwa Mkoa wa Dar Es Salaam.

Mafunzo hayo yamefunguliwa rasmi leo Jijini Dar Es Salaam na Waziri wa Afya Mheshimiwa Ummy Mwalimu na kuhusisha watoa huduma za afya kutoka Vituo vya kutolea Huduma za Afya vya Umma na Binafsi kutoka kona zote za Mkoa wa Dar Es Salaam.

Waziri Ummy amesema kuwa bado Ugonjwa wa Ebola uko nchini Uganda hivyo kutokana na ujirani wa nchi zetu kuna hatari ya Ugonjwa wa Ebola kuingia Tanzania huku Mkoa ambao uko hatarini zaidi ni Dar Es Salaam kutokana na kuwa ndio lango la shughuli za Uchumi na Biashara pamoja na Shughuli nyingine za kijamii.

“Mafunzo haya ya utayari wa kukabiliana na tishio la Ugonjwa wa Ebola kwa watoa Huduma za Afya zaidi ya 3,757 yatawawezesha watoa huduma kutambua mapema wagonjwa wa Ebola, kijikinga pamoja na kuwahudumia vyema wagonjwa” amesema Waziri Ummy Mwalimu.

Ameongea kuwa mafunzo hayo yanalenga kujiandaa kuokoa maisha ya watu lakini hatuwezi kuokoa maisha kabla ya kumlinda mtoa huduma za afya, kipaumbele chetu cha kwanza katika mapambano dhidi ya Ebola na magonjwa ya mlipuko ni kuwalinda Watumishi wa Afya”

“Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) tukilinganisha athari za Ugonjwa wa UVIKO-19 na Ebola, vifo vitokanavyo na UVIKO-19 ni chini ya asilimia 5, wakipata watu 100 vifo vinaweza kutokea 5. Kwa Ugonjwa wa Ebola vifo ni kwa asilimia 50 – 95. Kwa hiyo Ebola sio ugonjwa wa kuuchekea, tunashukuru Mungu hadi sasa hatujapata Mgonjwa lakini ni vyema tukajiandaa” Amesema Waziri Ummy

Waziri Ummy amesema ni matarajio yake mara baada ya watoa huduma hao kupata mafunzo watakuwa mstari wa mbele kutoa huduma za matibabu kwa wagonjwa wa Ebola endapo ugonjwa huo utaingia nchini.

“Matarajio yangu baada ya kupitia mafunzo haya mtaelewa vizuri namna ya kukabiliana na Ugonjwa wa Ebola, tukisema tumepata mgonjwa wa Ebola hamtomkimbia mgonjwa kwa sababu mmepata elimu, mbinu na uzoefu wa kumhudumia mgonjwa sitarajii kusikia mmemkimbia mgonjwa” amesema Waziri Ummy.

“Serikali ya Awamu ya Sita itaweka kipaumbele cha juu kuwalinda watoa Huduma za Afya hususani walio mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya magonjwa ya mlipuko” Amesema Waziri Ummy Mwalimu na kumshuruku Rais Samia Suluhu Hassan kwa usimamiaji mzuri wa Sekta ya Afya kwa kuhakikisha tunajiandaa kukabiliana na mlipuko wa Ugonjwa wa Ebola ambao umetoka katika nchi jirani ya Uganda.

Aidha, Waziri Ummy amewaomba wananchi kutopuuzia na kudharau tetesi yeyote ya mgonjwa wa Ebola, huku akiwaomba endapo wakisia tetesi yeyote kutoa taarifa ili ifanyiwe kazi na kuongezea kuwa uwezo wa kupima na kugundua Ugonjwa wa Ebola tunao hapa nchini.

Kwa upande wake Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Afya Duniani nchini Tanzania Dkt. Zabron Yoti amesema kuwa Watashirikiana na Serikali katika utayari wa kukabiliana na Ugonjwa huo hatari kwa kusaidia kuratibu utoaji wa mafunzo ambayo yatawajengea uwezo watoa huduma kufanya kazi kwa ufanisi pamojaa na kuwapa vitendea kazi na usimamizi mzuri ili waweze kufanya kazi kwenye mazingira salama.

“Ulinzi kwa watoa huduma za afya ni kipaumbeke muhimu kwetu sote, Serikali pamoja na wadau wote tushirikiane kukabiliana na Ugonjwa wa Ebola” amesisitiza Dkt. Yoti.

Naye, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam Dkt. Rashid Mfaume ameshukuru Serikali, WHO pamoja na wadau wengine wa Sekta ya Afya kuweka kipaumbeke kwenye kukinga wananchi dhidi ya Ugonjwa huo na kuwajengea watoa huduma za afya utayari wa kukabiliana na Ugonjwa wa Ebola.

“Haijawahi kutokea ndani ya Mkoa wa Dar Es Salaam zaidi ya watoa Huduma za Afya 3,757 kupata mafunzo haya muhimu ya kukabiliana na Ugonjwa wa Ebola kwa wakati mmoja, tunashukukuru Waziri Ummy Mwalimu kwa maamuzi haya ya kuwajengea uwezo wa utayari watoa huduma za afya kukabiliana na Ugonjwa wa Ebola” amesema Dkt. Mfaume.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here