Na:Faustine Gimu ,Dodoma.
Waandishi wa Habari wametakiwa kuweka kipaumbele kuandika habari za kuelimisha jamii namna ya kujikinga na magonjwa ya mlipuko ikiwemo UVIKO-19 pamoja na kuhamasisha umuhimu wa chanjo.
Wito huo umetolewa leo Novemba 4.2022 jijini Dodoma na Afisa afya jiji la Dodoma Thobias Kigwinya wakati akitoa mafunzo ya kuwajengea uelewa wanahabari Mkoa wa Dodoma namna ya kuripoti habari zinazohusu magonjwa ya mlipuko ikiwemo Uviko-19 yaliyoandaliwa na Taasisi ya Habari ya Internews.
Afisa afya huyo amesema wanahabari wana mchango mkubwa katika katika kuelimisha jamii katika uhamasishaji wa kujikinga na magonjwa ya mlipuko na umuhimu wa utumiaji wa chanjo hivyo ni wajibu kwa kila mwanahabari kuandika habari zenye usahihi na zisizokuwa na mkanganyiko kwa jamii juu ya magonjwa ya mlipuko.
Hata hivyo Kigwinya ameendelea kuwahakikishia wanahabari kuendelea kushirikiana na wataalam wa afya katika kuelimisha kuhamasisha jamii umuhimu wa chanjo ya uviko-19 kwani ni salama na haina madhara yoyote.
“Chanjo ya Uviko-19 ni salama na haina madhara yoyote ,inapunguza madhara ya ugonjwa huo hivyo chanjo sio kitu cha kubeza wanahabari tusaidiane kutoa elimu sahihi kwa jamii”amesema.
Akizungumzia maadili ya uandishi wa Habari za magonjwa ya mlipuko ikiwemo Uviko-19 Mjumbe wa Bodi Umoja wa Klabu ya Waandishi wa Habari Tanzania[UTPC] Yusuph Musa amesema ni muhimu kuzingatia uadilifu,na usahihi wa taarifa pamoja na kuzingatia usiri wa taarifa.
“Unakuta watu hawana uelewa kuhusu chanjo unaandika kichwa cha habari wananchi wagomea chanjo badala ya kuandika wananchi wahitaji uelewa kuhusu chanjo hivyo ni muhimu sana kuzingatia maadili ya uandishi “amesisitiza.
Nao baadhi ya waandishi wa Habari wahamasishaji wa chanjo ya Uviko-19 mkoa wa Dodoma akiwemo Bilson Vedastus pamoja na Bahati Msanjila wamesema ni muhimu kutumia vyanzo vya kuaminika na kuzingatia uzalendo kuhusu habari za chanjo na magonjwa ya mlipuko.
“Katika suala la uandishi unapoandika habari za Uviko-19 na magonjwa ya mlipuko jitahidi sana kuangalia vyanzo vya kuaminika mfano tovuti ya wizara ya Afya ,pia ni muhimu kuangalia mambo kwa kina ,uzalendo,habari isilete taharuki na kuangalia vyanzo vingine vya taarifa vinavyoaminika”amesema Bilson.
“Ni muhimu kuepuka lugha za kuogofya na kuzingatia maudhui na panahitaji kuwepo kwa mjadala kuwajengea uelewa wananchi “amesema Msanjila.