WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imesitisha kwa muda wa miezi mitatu zoezi la utambuzi wa mifugo kwa kutumia hereni za kielektroniki wakati ikiendelea na tathmini ambayo itawezesha kutoa muongozo wa namna bora zaidi ya kutekeleza zoezi hilo.
Mheshimiwa Majaliwa amesema bei elekezi ya kuweka hereni za kielektroniki kwa mnyama mmoja ni shilingi 1,750 kwa ng’ombe na punda na shilingi 1,000 kwa mbuzi na kondoo. ’’Gharama hizi zimekuwa zikilalamikiwa na wafugaji kuwa ni kubwa tofauti na uhalisia.’’
’’Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan imesikia hoja za wafugaji kuhusu mapungufu ya kanuni, usimamizi wake na utekelezaji wake na gharama kubwa za uwekaji hereni za kielektroniki na inaona kuna haja ya kufanya upya tathmini ya zoezi hilo.’’
Ameyasema hayo leo (Alhamisi, Novemba 3, 2022) Bungeni jijini Dodoma wakati akitoa ufafanuzi kuhusu utekelezaji wa zoezi la utambuzi wa mifugo kwa kutumia hereni za kielektroniki na kuzuka kwa moto katika hifadhi ya Taifa ya Kilimanjaro.
Amesema kuwa zoezi la utambuzi wa mifugo kwa kutumia hereni za kielektroniki lilipaswa kukamilika tarehe 31 Oktoba, 2022 lakini hadi kufikia tarehe hiyo idadi ya mifugo iliyotambuliwa na kusajiliwa ni 5,068,617 sawa na asilimia 11 ya lengo la kutambua mifugo 45,920,000.
Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema Serikali haijasitisha malipo kwa ajili ya huduma hiyo bali wamesitisha zoezi linalolalamikiwa ili kuipa nafasi Serikali kupitia Wizara ya Mifugo kufanya tathmini ya mapungufu ya kikanuni yaliyowekwa kwa ajili ya kufanikisha zoezi hilo vizuri kwa kushirikisha wadau wa mifugo.
Amesema Serikali imefanya juhudi kubwa kuibadili sekta hiyo kwa kufungua soko la nyama katika nchi mbalimbali, kuondoa tozo kero na kuweka ruzuku kwenye dawa za kuogeshea mifugo na ujenzi wa mabwawa na malambo. ’’Natoa wito kwa wafugaji wote nchini kufuga kisasa ili kuwa na uhakika wa upatikanaji wa nyama na mazao mengine kwa ajili ya masoko na uchakataji wa ndani na nje ya nchi.’’
Pia, Mheshimiwa Majaliwa ameziagiza Wizara za Maji, Mifugo na Uvuvi na Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya mifugo kuhakikisha miradi mikubwa ya maji inayotekelezwa kwenye maeneo yenye shughuli za wafugaji inafanyiwa tathimini na kupewa kipaumbele cha kutengeneza miundombinu kwa ajili ya mifugo ikiwemo maeneo ya kunyweshea badala ya kuiacha mifugo kwenda kwenye mabonde yaliyohifadhiwa.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu ametoa maagizo matatu kwa Wizara ya Maliasili na Utalii na TANAPA katika kukabiliana na changamoto ya moto kwenye maeneo ya hifadhi ikiwemo mlima Kilimanjaro wakati inapojitokeza.
’’Hakikisheni mnaunda kitengo ndani ya TANAPA cha kukabiliana na majanga au maafa yanayotokea ndani ya hifadhi. Pia wekezeni kwenye matumizi ya teknolojia ya kisasa hususan katika tahadhari, utambuzi na uzimaji moto pamoja na kuimarisha shughuli za doria na uokoaji kwa kushirikisha jamii na wadau.’’
Kadhalika, Waziri Mkuu amesema Serikali itaendelea kuboresha uwezo wa kupambana na majanga kwa kuimarisha sheria za mifumo ya kitaasisi na kutoa mafunzo ya pamoja miongozi mwa vyombo ndani na nje ya nchi. Pia wakati wote itahakikisha upatikanaji wa vifaa vya tahadhari, uokozi na kutoa huduma mapema kwa waathirika.
Mheshimiwa Majaliwa ametumia fursa hiyo kutoa shukrani kwa Wizara ya Maliasili na Utalii, Mkoa wa Kilimanjaro, Majeshi, TANAPA, taasisi nyingine za Serikali pamoja na zisizo za Serikali, wananchi wa vijiji vya jirani na hifadhi pamoja na wadau wote walioshiriki kikamilifu katika uzimaji wa moto.
 (mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKU
S. L. P. 980, 41193 – DODOMA
ALHAMISI, NOVEMBA 3, 2022.