-Yanahitajika kwa Wingi Duniani
-Migodi Yatoa Ajira kwa Watanzania
Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa amebainisha kuwa, biashara ya Makaa ya Mawe inatarajia kuleta tija kwa Watanzania kutokana na uhitaji mkubwa wa madini hayo ndani na nje ya nchi.
Dkt. Kiruswa ameeleza hayo Novemba 12, 2022 wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma alipotembelea mgodi wa uchimbaji wa Makaa ya Mawe wa Ruvuma Coal Ltd ili kujionea shughuli za uchimbaji zinazoendelea katika mkoa huo.
Ameeleza kuwa, Serikali imeweka mazingira wezeshi ya uwekezaji katika Sekta ya Madini yanayovutia wawekezaji kutoka nchi mbalimbali duniani kuja kuwekeza na kufanya biashara ya madini mbalimbali yakiwemo Makaa ya Mawe.
Aidha ameongeza, Serikali itaendelea kuboresha miundombinu ya barabara ili kurahisisha usafirishaji wa Makaa ya Mawe kutoka kwenye migodi hususan barabara ya kuelekea mkoani Mtwara ili kusafirisha Makaa ya Mawe hayo katika bandari.
“Katika mikoa yote yanapochimbwa Makaa ya Mawe mnakaribishwa katika mkutano maalum utakaowasaidia kupata uelewa sahihi wa makaa ya mawe na madini mengine yanayopatikana katika mkoa huo na maeneo jirani,” amesema Dkt. Kiruswa.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mbinga, Aziza Mangosongo amesema, kutokana na uwepo wa migodi imesaidia wilaya hiyo kupata faida nyingi katika kutekeleza shughuli za kijamii ikiwemo ujenzi wa shule na vituo vya afya.
Amesisitiza wadau wa Makaa ya Mawe katika wilaya hiyo kushiriki mkutano ulioandaliwa na Wizara ya Madini ili kujifunza uwajibikaji wa makampuni kwa jamii (CSR) katika siku zilizopangwa ili kupata uelewa zaidi.
Naye, Mbunge wa Jimbo la Mbinga Vijijini, Benaya Kapinga amesema Makaa ya Mawe yanahitajika kwa wingi duniani kwa sasa.
Amesema Serikali itumie fursa hiyo kuhakikisha wilaya inapata faida ya uwepo wa migodi kwa kutoa ajira na kuleta maendeleo kwa jamii zinazozunguka mgodi hiyo.
Naye, Meneja Mkuu wa Mgodi wa Makaa ya Mawe Ruvuma, Benedicto mshingwe amesema, hadi sasa mgodi huo umetoa ajira zaidi ya 700 kwa Watanzania hususan wanaozunguka mgodi. Pia, amesema mgodi umeendelea kushiriki katika shughuli za kijamii ikiwemo ujenzi wa madarasa na zahanati ili kujenga mahusiano mazuri.
Awali, Dkt. Kiruswa amekutana na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Laban Thomas na wadau mbalimbali wa sekta ya Madini na kuzungumzia shughuli za uchimbaji madini zinazofanyika katika mkoa huo na changamoto wanazopitia.