Home Uncategorized SUA YATENGEWA BIL. 73.6 KUBORESHA ELIMU

SUA YATENGEWA BIL. 73.6 KUBORESHA ELIMU

NA: FARIDA MANGUBE MOROGORO.
Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo mkoani Morogoro kimetengewa shilingi Bilioni 73.6 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu mbalimbali kupitia mradi wa  Elimu ya Juu kwa Mabadiliko ya Kiuchumi (HEET)  kwa lengo la kuboresha mazingira ya kufundishia na kuendana na soko la ajira.
Kupitia mradi huo Chuo kimeandaa mpango maalumu wa kujenga miundombinu mipya  katika kampasi ya Edward Moringe Sokoine, Solomon Mahlangu na Mizengo Pinda kwa lengo la kuinua uchumi.
Akizungumza kwenye mahafali ya 40 yaliyofanyika katika Kampasi kuu ya Edward Moringe Sokoine Mjini Morogoro. Makamu Mkuu wa Chuo  Prof. Raphael Chibunda, alisema kupitia mradi huo Chuo kitajenga majengo 11 kwa ajili ya kujifunzia na kufundishia na kwamba katika Kampasi ya Edward Moringe  yatajengwa majengo mapya 6, Solomon Mahlangu 2 na Mizengo Pinda yatajengwa 3.
Majengo hayo ni pamoja na Hosteli 3, ofisi 3 za taaluma, maabara 3, tahalia 1 na jengo 1 kwajili ya kukuza utafiti na ubunifu katika nyanja za uhandisi na tehema.
“Mradi huu pia utasaidia katika kuboresha mitaala, ununuzi wa vitabu na uboreshaji wa mafunzo kwa watumishi.” Alisema Prof. Raphael Chibunda Makamu Mkuu wa Chuo.
Aidha alisema, upanuzi wa Kampasi ya Mizengo Pinda unaendelea ambapo mpaka kufikia mwezi Oktoba, Chuo kimetumia kiasi cha Shilingi Bilioni 1.6 kwa ajili ya shuhuli za ujenzi na ukarabati katika Kampasi hiyo.
Pia Chuo kimeendelea kufanya tafiti mbalimbali pamoja na kuwajengea uwezo watafiti wachanga kwa lengo la kuwaongezea ujuzi ili waweze kutafiti na kutafuta majawabu ya changamoto zinazojitokeza.  Chuo kimetoa shilingi milioni 500 kwaajili ya kuwajengea uwezo watafiti wachanga 34.
  
Kijana Michael Jackson ni miongoni mwa wahitimu 176 wa shahada ya kwanza ya Misitu Chuo Kikuu cha Sokoine cha Killimo, akizungumza na Michuzi Blog alisema pamoja na kutambua wazi kwamba changamoto ya kutokuwepo kwa uhakika wa ajira, bado analotumaini la kujikwamua kimaisha kupitia taaluma yake.
Alisema tatizo la ukataji miti kiholela ni chanzo cha ongezeko la joto ikichagiwa na mabadiliko ya hali ya hewa, hivyo hamasa ya mapambano dhidi ya kudhibiti vitendo vya uharibifu wa mazingira itasaidia kunusuru upotevu wa miti asilia pamoja na viumbe.
Jackson alisema, analitazama tatizo la ukataji miti kuwa fursa, kufanikisha ndoto kwa kuungana na vijana wengine katika kushiriki harakati za kupinga uharibifu wa mazingira ambayo imepelekea upotevu wa miti asilia.
Aidha alisema, matarajio yake ni kuanzisha kituo cha bustani kama shamba darasa pamoja na kutoa huduma za kibiashara, mpango ambao anautama kuwa na fursa pana kwenye soko la ajira mjini na vijijini.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here