SERIKALI imeendelea kujipanga kuhakikisha inadhibiti kuingia kwa maambukizi ya Virusi vya Ebola nchini kwa kuhakikisha inaanda mipango madhubuti katika maeneo ya uwanja wa ndege pamoja na maeneo ya mipaka ambapo wameweka wataalamu kwaajili ya kuhakikisha wanaoingia nchini wanafatiliwa kwa uangalizi.
Akizungumza leo Novemba 14,2022 Jijini Dar es Salaam Mratibu wa Ufuatiliaji na Udhibiti wa Magonjwa, Dkt.Vida Makundi wakati akifungua Mafunzo kwa Waahudumu ngazi ya jamii ambao kazi yao itakuwa kuwafuatilia wale ambao watakuwa wamekutana na wagonjwa wa Ebola na kutoa taarifa.
Amesema katika harakati za kujiandaa kuzuia na kudhibiti ugonjwa wa Ebola, wanajiandaa pia katika zoezi la kufuatilia watu waliotangamana na mgonjwa wa Ebola endapo kwa bahati mbaya atakuwa amepatikana.
“Ufuatiliaji wa wasafiri ambao wametoka Uganda na sehemu nyingine ambao wanaweza wakawa wamekutana na wagonjwa tunawafuatilia kwa kuwahoji kila siku kama wanadalili zozote ambazo zinafanana na kuwa na dalili za Ebola”. Amesema
Amesema kuwa inaaminika mgonjwa wa Ebola kama amekutana na mtu kati ya siku mbili mpaka siku 21 kama mtu amepatwa na maambukizi ndipo atakapoona dalili hivyo wanafundisha makundi mbalimbali ya wafuatiliaji.
Hata hivyo amesema Wahudumu ngazi ya jamii watakuwa wanatumika endapo ikahitajika kuwafuatilia wale ambao wamekuwa wamekutana na wagonjwa na watakuwa wanatoa taarifa kwa viongozi wao ambao ni Maafisa Afya ndani ya kata ambao watakuwa wanatoa taarifa kwenye halmashauri zao.
Aidha amesema wahudumu ngazi ya jamii pia watakuwa wakifuatilia tetesi za magonjwa ndani ya jamii, wakipata tetesi ya mgonjwa yeyote ambaye yanaonekana yanaambukiza, yanahatari ya kuambukiza wanatoa taarifa kituo chochote cha afya kilichopo karibu au kwa afisa afya ngazi ya kata na taarifa zinakwenda juu kwaajili ya uchunguzi.