Naibu Waziri, Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara Mhe. Exaud Kigahe (Mb) amesema kuwa Serikali inatambua mchango wa Wafanyabiashara Nchini na Kuthamini tuzo za Chaguo la Mteja Afrika (CCAA) ambazo zinaleta mchango mkubwa kwa Taifa kupitia maoni ya walaji ambao ndio watumiaji wenyewe wa huduma mbalimbali.
Mhe. Kigahe ameyasema hayo tarehe 12 Novemba, 2022 katika hafla ya utoaji tuzo kwa Makampuni mbalimbali yanayotoa huduma kwa wananchi katika ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es salaam.
“Serikali ya awamu ya sita imeendelea kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara kwa kufuta tozo na kufanya marekebisho ya sheria mbalimbali hivyo tuzo hizi zinaongeza ushindani wenye nia ya kuboresha na kuongeza uzalishaji wa bidhaa na utoaji huduma. Amesema Mhe. Kigahe.
Mkurugenzi wa Lavine International Agency Limited, Diana Laizer ambao ndio waandaaji wa tuzo za Chaguo la Mteja Afrika (CCAA) amesema kuwa tukio la utoaji tuzo za biashara linatambua, linaboresha na kukuza ubora wa biashara kupitia chaguo la watumiaji na kuna vipengele ambavyo vinahusisha makampuni na wafanyabiashara ambao siyo watanzania, ambao vinagusa ukanda wa Afrika Mashariki, Afrika Magharibi na Afrika Kusini.
Tuzo za Chaguo la Mteja Afrika 2022 (CCAA) ambazo zilianzishwa mwaka 2019 chini ya shirika la Lavine International Agency Limited na washirika rasmi wa tuzo hizi ni TANTRADE, AZAM TV na Auditax International ambao ni mfumo wa upigaji kura unaothibitisha CCAA 2022.
Tuzo hizi zimehudhuriwa na watu mbalimbali mashuhuli akiwemo mgeni maalumu mualikwa ambaye ni mwanamitindo na muigizaji kutoka Nchini Nigeria Iniobong Edo Akim maalufu kama IniEdo.