Home LOCAL RUWASA YAELEZA MIKAKATI YAKE HUDUMA YA MAJI VIJIJINI 

RUWASA YAELEZA MIKAKATI YAKE HUDUMA YA MAJI VIJIJINI 

Mkurugenzi Mkuu wa RUWASA, Mhandisi Clement Kivegalo

WAKALA wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) umeeleza, katika mwaka wa fedha 2022/23, wakala huo upanga kutekeleza miradi 1,029, kati ya hiyo, miradi hiyo 381 ni mipya, miradi 648 utekelezaji wake unaendelea kutoka mwaka wa fedha uliopita.

Ni kauli ya Mhandisi Clement Kivegalo, Mkurugenzi Mkuu wa RUWASA aliyoitoa mbele ya baadhi ya wahariri jijini Dar es Salaam wakati akizungumzia utendaji kazi wa taasisi hiyo.

RUWASA na wahariri walifanya kikao hicho tarehe 1 Oktoba 2022 ambapo Pamoja na mambo mengine, wakala huo ulieleza mikakati yake katika kutoa huduma bora kwa wananchi.

“Kukamilika kwa miradi hii, kutaongeza upatikanaji huduma za maji vijijini hadi kufikia asilimia 85 mwaka 2025, mwaka 2022/23, Serikali imetenga sh. bilioni 889.2 za ujenzi wa skimu za maji vijijni,” alieleza.

Akizungumza na wahariri hao, Mhandisi Kivegalo alisema, hadi Julai 2019 upatikanaji huduma ya maji vijijini ulikuwa asilimia 64.8, pamoja na kiwango hicho hali ya huduma ya maji vijijini haikuwa ya kuridhisha.

‘‘Baadhi ujenzi wa miradi ya maji ilichukua muda mrefu ambapo miradi iliyokuwa ikikamilika, kuzinduliwa, ilidumu muda mfupi na kusababisha wananchi wa vijijini kupata adha ya maji.

“Miradi hiyo ilikuwa ikijengwa kwa gharama kubwa ikilinganishwa na uhalisia,” aliongeza. Kwa sasa, kati ya vijiji vyote nchini 12,319, vijiji 9,029 tayari vimefikiwa na huduma ya maji safi na salama.

“Hadi Juni, 2022, hali ya upatikanaji huduma ya maji vijijini imefikia asilimia 74.5, huduma inapatikana kupitia vituo 143,767 vya kuchotea maji, na muunganisho wa majumbani 169,043,” alisema.

Mhandisi Kivegalo alisema, kasi hiyo ni nzuri, wanatarajia kuvuka lengo la asilimia 85 ifikapo mwaka 2025, kama ilivyoelekezwa na Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Alieleza kuwa, kutokana na umuhimu wa kazi ambazo zinafanywa na RUWASA, serikali iliongeza uwezeshaji rasilimali fedha ili kuongeza kasi ya kuwapatia wananchi waishio vijijini huduma endelevu ya maji safi na salama.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here