Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la nyumba la Taifa (NHC) Neemia Mchechu amesema kuwa kuzinduliwa kwa sera ya ubia kutawezesha utekelezaji wa miradi mbalimbali kwa wakati inayosimamiwa na shirika hilo.
Mchechu ameyasema hayo leo Novemba 16,2022 Jijini Dar es Salaam katika mahojiani na waandishi wa habari mara baada ya kumalizika kwa hafla ya uzinduzi wa sera ya ubia ambapo Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alikuwa mgeni rasmi.
Amesema sera hiyo itasaidia kuwavutia wawekezaji kutoka nje ya nchi pamoja na kuchochea kuongezeka kwa kasi ya ujenzi wa nyumba kwa lengo la kupunguza mahitaji ya nyumba nchini.
“Sera hii inakwenda kuamsha uwekezaji mkubwa hapa nchini pamoja na kutia hamasa mpya katika kupunguza mahitaji ya nyumba nchini kutokana na Sekta Binafsi kuweza kupata maeneo ya uwekezaji kiurahisi”
“Pia Sera itatoa fursa kwa NHC kuingia ubia na Sekta Binafsi kujenga miradi ya maendeleo katika viwanja vinavyomilikiwa na Shirika” amesema Mchechu.
Aidha ameongeza hatua hiyo inaunga mkono maelekezo ya Rais Samia Suluhu kuruhusu Sekta Binafsi kuwekeza mitaji ili kujenga uchumi wa Taifa.