Home LOCAL MKOA WA DAR ES SALAAM WAPOKEA VIFAA KINGA KUTOKA WATERAID TANZANIA KWA...

MKOA WA DAR ES SALAAM WAPOKEA VIFAA KINGA KUTOKA WATERAID TANZANIA KWA AJILI YA KUKABILIANA NA JANGA LA EBOLA

Mganga Mkuu wa  Mkoa wa Dar es Salaam Dkt.Rashid Mfaume(wa tatu kulia) akikabidhiwa moja ya kasha lenye vifaa kinga kutoka kwa Mshauri wa Sera na Uraghabishi wa Shirika la WaterAid Tanzania Christina Mhando(wa pili kushoto).Wa kwanza kushoto ni Ofisa Afya Mkoa wa Dar es Salaam Enezael Ayo.Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Dk.Rashid Mfaume akizungumza baada ya kupokea msaada wa vifaa kinga mbalimbali kutoka kwa Shirika la Kimataifa la WaterAid Tanzania.Wa kwanza kushoto ni Mshauri wa Sera na Uraghabishi wa Shirika la WaterAid Tanzania Christina Mhando na katikati ni Ofisa Afya Mkoa wa Dar es Salaam Enezael Ayo.
Maofisa kutoka shirika la WaterAid Tanzania pamoja na maofisa wa Serikali Ofisi ya Mkoa wa Dar es Salam wakiangalia takwimu za vifaa kinga kabla ya kufanyika kwa makabidhiano ya vifaa hivyo.
Mshauri wa Sera na Uraghabishi wa Shirika la WaterAid Tanzania Christina Mhando(kulia) akielezea sababu za kuona umuhimu wa kutoa msaada wa vifaa kinga kwa kwa Mkoa wa Dar es Salaam ajili ya kujikinga na magonjwa mbalimbali ya mlipuko ukiwemo ugonjwa wa Ebola ambao uko kwenye nchi jirani ya Uganda.
Baadhi ya makasha yenye vitasa mikono yakiwa katika Ofisi ya Mkoa wa Dar es Salaam baada kukabidhiwa na Shirika la Kimataifa la WaterAid.Ofisa Mawasiliano na Kampeni wa Shirika la WaterAid Tanzania Neema Kimaro akipanga baadhi ya makasha ya vifaa kinga ambavyo wamekabidhi kwa  Mkoa wa Dar es Salaam kwa lengo la kukabiliana na magonjwa ya  mlipuko hasa ebola  ambao unaelezwa kuwa uko kwe ye nchi jirani ya Uganda.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Dk.Rashid Mfaume(kulia) Mshauri wa Sera na Uraghabishi wa Shirika la WaterAid Tanzania Christina Mhando (katikati) na Ofisa Afya Mkoa wa Dar es Salaam Enezael Ayo(kushoto) wakijadiliana jambo. (Picha na Said Mwishehe, Michuzi TV).
OFISI ya Mkoa wa Dar es Salaam imepokea msaada wa vifaa kinga kutoka Shirika la WaterAid Tanzania kwa lengo la kuendelea kushirikiana na Serikali kukabiliana na magonjwa ya mlipuko ukiwemo wa Ebola ambao unatajwa kuwepo nchi jirani ya Uganda.
Vifaa kinga hivyo ambavyo ni sabuni, vitakasa mikono na barakoa vimekabidhiwa leo Novemba 4 mwaka 2022 kwa Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Dk.Rashid Mfaume na kushuhudiwa na maofisa mbalimbali wa ofisi ya Mkoa huo pamoja na WaterAid Tanzania.
Akizungumza baada ya kupokea msaada wa vifaa kinga kutoka WaterAid Tanzania, Dk.Mfaume amesema wameendelea kuchukua hatua mbalimbali za kukabiliana na magonjwa ya mlipuko ukiwemo wa Ebola ambao upo nchini ya Uganda huku akifafanua kuwa hadi sasa Dar es Salaama na nchi kwa ujumla hakuna mgonjwa wa Ebola.
“Tunashukuru kwa msaada huu ambao umetolewa na wadau wetu muhimu WaterAid, nasema ni wadau muhimu kwasababu wamkuwa pamoja nasi nyakati zote na tumekuwa tukipokea misaada yao mingi yenye lengo la kushirikiana nasi kukabiliana na magonjwa ya mlipuko.
“Vifaa kinga ambavyo tumevipokea tutakwenda kubikabidhi kwenye maeneo yenye mikusanyiko ya watu na moja eneo ambalo tutapeleka msaada huu ni Stendi ya Magufuli pale Mbezi Mwisho.Tunaamini kwa pamoja tutaweza kukabiliana na magonjwa ya mlipuko na sisi kama mkoa tunaendelea kuchukua hatua mbalimbali ili kuhakikisha wananchi wanabaki salama,”amesema Dk.Mfaume.
Aidha ameshauri wananchi kuendelea kuzingatia usafi ikiwa pamoja na kujenga utamaduni wa kunawa mikono mara kwa mara ili kuejipusha na vijijidu ambavyo vinasababisha magonjwa ya mlipuko huku akisisitiza jukumu la kulinda afya ni la kila mmoja wetu.Kwa upande wake Mshauri wa Sera na Uraghabishi wa Shirika la WaterAid Tanzania Christina Mhando amesema wamekuwa wakichukua hatua mbalimbali kushirikiana na Serikali kupitia Wizara ya Afya katika kukabiliana na magojwa mbalimbali.
“Sisi kama shirika la WaterAid Tanzania tulichukua nafasi ya siku ya maadhimisho ya unawaji mikono duniani ili kuungana na Wizara ya Afya chini ya uongozi madhubuti wa Rais Samia Suluhu Hassan kutoa hiki kidogo ili kiwe kama mbegu na kichochezi kwa wadau wengine kuungana pamoja na Serikali katika kujikinga dhidi ya ugonjwa wa Ebola.
“Tulichukua hatua ya kuwasiliana na Wizara ya Afya na kuona ni namna gani tunaweza kuunga mkono juhudi za Serikali kukabiliana na hili janga la Ebola ambao uko kwa majirani zetu ili usiweze kuingia kwetu. Wizara walitupatia orodha ya vifaa kinga na pia walielekeza kuvileta ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam siku ya leo,”amesema.
Ameongeza kuwa  kama wanavyofahamu mkoa huo ni mmoja ya mikoa mitano iliyo hatarini na ugonjwa wa Ebola nchini Tanzania kutokana na mwingiliano wa watu.Hivyo basi WaterAid Tanzania wamekabidhi vifaa kinga hivyo vyenye thamani ya Sh.milioni tano kwa uongozi wa ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam.
“Vifaa hivi ni sabuni za kunawia mikono dozen 45, vitakasa mikono(sanitizer) dozen 24, gloves dozen 5 pamoja na masks dozen 10.Tunatambua Oktoba 31 mwaka huu Waziri wa Afya Ummy Mwalimu alitoa rai kwa wadau kushirikiana na Serikali kutoa vifaa kinga kwa wataalamu ili kujikinga na ugonjwa wa Ebola ambao unazidi kusambaa nchini Uganda.
“Ambapo  mpaka sasa ugonjwa wa Ebola umeingia Kampala na Entebbe na kuongeza kuwa ndege zinazokuja kutoka Kampala, kuja Dar es Salaam na mabasi kunaiweka Tanzania katika hatari ya kupata mlipuko huu kutokana na mwingiliano mkubwa wa kiuchumi na kijamii na Uganda. 
“Shirika la WaterAid lina lengo la kuhakikisha kila mtanzania anapata maji safi na salama, siha binafsi pamoja na usafi wa mazingira na kubwa zaidi anapata huduma hizi ifikapo mwaka 2030 na linakuwa ni jambo la kawaida kwa kila mtanzania.
“Tunaamini kuwa yote haya yanawezekana kwa kupitia ushirikiano, kutekeleza kwa kuonyesha mfano, na kutumia yale mazuri tuliyojifunza kujengea uwezo watendaji na kutumika katika kufanya maamuzi katika ngazi mbalimbali. Lakini pia  kutanguliza mbele masuala ya kijinsia, kama vile tunavyofahamu wanawake na wasichana, iwe kwenye vituo vya kutolea huduma za afya, mashuleni na majumbani, mara nyingi hubeba mzigo mkubwa wa athari za ukosefu maji safi na salama, siha binafsi pamoja na usafi wa mazingira.”

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here