Home BUSINESS MHE. HAMAD AKITAKA CHUO CHA MIPANGO KUFUNGUA TAWI LAKE VISIWANI ZANZIBAR

MHE. HAMAD AKITAKA CHUO CHA MIPANGO KUFUNGUA TAWI LAKE VISIWANI ZANZIBAR

Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini kimetakiwa kuongeza wigo wa utoaji wa huduma zake kwa kufungua Tawi la chuo hicho Visiwani Zanzibar.

Wito huo umetolewa na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mheshimiwa Hamad Chande wakati alipotembelea banda la Chuo hicho kwenye Maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha yanayoenda sambamba na maonesho yanayofanyika katika viwanja vya Rocky City Mall jijini Mwanza.

Naibu Waziri huyo amepongeza kazi kubwa inayofanywa na Chuo cha Mipango kwa kufundisha Kozi ambazo wataalam wake wanahitajika katika utekelezaji wa mikakati ya Serikali ya kuleta maendeleo na ustawi wa maisha ya watanzania.

“Kozi zenu ni nzuri kwa sababu mmekuwa mkituandalia wataalam muhimu kwa maendeleo ya Nchi yetu. Sasa kwa kuwa Chuo hiki kipo chini ya Wizara ya Fedha na Mipango ambayo ni Wizara ya Muungano, hivyo ni muhimu kuangalia uwezekano wa kufungua Tawi la Chuo kule Visiwani Zanzibar ili kutoa fursa kwa Wazanzibar wengi kujiunga na kusomea kozi hizi”, alisema Naibu Waziri Chande.

Aidha, Mheshimiwa Chande alipongeza hatua ya Chuo cha Mipango kujumuisha somo la Ujasirimali katika kozi zake kwa kuwa hatua hiyo inawaandaa wahitimu wake kujiajiri wenyewe badala ya kusubiri kuajiriwa mara baada ya kuhitimu.

Katika hatua nyingine, banda la Chuo cha Mipango lilitembelewa na wadau mbalimbali akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Busega, Bw. Gabriel Zakaria, pamoja na wanafunzi wa Chuo cha Rians Empowerment Center kinachotoa mafunzo ya Ujuzi Kazi kilichopo jijini Mwanza.

Maadhimisho hayo ya Wiki ya Huduma za Fedha yalifungliwa rasmi jana Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Phillip Isdor Mpango.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here