Na: Mwandishi Wetu
MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam Amos Makala amesema mgogoro wa ardhi unaoendelea Kimbiji Manispaa ya Kigamboni umetengenezwa na wataalam wa ardhi wa Manispaa hiyo.
Akizungumza jana baada ya ziara kukagua maeneo yenye mgogoro huo wa barabara, Makala alisema picha aliyoipata ni wataalam wa idara ya ardhi kuanzisha mgogoro kwa kuwa ndio wahusika waliotoa hati za viwanja kwenye maeneo hayo.
“Kuona ni kuamini, nimesikia mengi sana yakisemwa kuhusu mgogoro huu, nimekuja mwenyewe nimejionea, ni wazi baada ya kusikia pande zote na vielelezo wataalamu wetu wa ardhi ndio wametufikisha hapa,” alisema Makala.
Aidha, alisema busara pekee ndio inaweza kuumaliza mgogoro huo uliodumu muda mrefu.
“Sasa naagiza. natoa siku saba Manispaa mumtafute huyu muwekezaji ASM pamoja na walalamikaji wa hii barabara tukae kikao cha pamoja ambacho mimi mwenyewe nitakiendesha tutafute suluhu ya ili jambo, kwani kuna shida gani huyu ASM akiamua kuvunja ukuta kuruhusu barabara ipite, ni busara tu!?, nipo tayari kuvunja ratiba ya siku nzima kukaa kwenye hiko kikao,” alisema Makala.
Mgogoro huo ulioanza mwaka 2015 umetokana na mwekezaji (ASM ) kuziba barabara inayotumiwa na wananchi na wawekezaji wengine kufika kwenye maeneo yao na Pwani ya bahari.
ASM anamiliki viwanja viwili pacha ambavyo vimetengeshwa na barabara inayoelekea kwenye viwanja vya wawekezaji wengine.
Kabla ya makala kufanya ziara kwenye maeneo hayo ya mgogoro, tayari maamuzi yalitolewa na Wizara ya Ardhi kuitaka Manispaa ya Kigamboni kufanya tathimini na kumlipa fidia mwekezaji ASM ili kuruhusu barabara hiyo kutumika, tathimini hiyo ilifanyika na ASM kutakiwa kulipwa shilingi milioni 126.
Hata hivyo katika kikao cha kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya hiyo ilitoa maamuzi mengine ya Kuchukua sehemu ya viwanja vya wananchi na kuwalipa fidia kupisha barabara mchepuko.
Hatua hiyo imeleta mvutano mkubwa huku wananchi wakishangazwa na maamuzi hayo ya pili ya kuchukua sehemu ya maeneo yao.
Mmoja wa wakazi ambaye shamba lake linatakiwa kumegwa kwa ajili ya barabara, Mzee Mwinyipingu Mbwana, alisema tayari maamuzi ya kumlipa mwekezaji ASM yalishafanyika na tathimini ilifanyika sasa wanashangaa Manispaa kuja na maamuzi mapya.
” Tunakushuru sana mkuu wa Mkoa kwa kuja kujionea mwenyewe, na bahati nzuri mwenyewe umekiri kuwepo kwa madudu kwa wataalam wetu, tunaomba kama ulivyoahidi utusaidie kuumaliza mgogoro huu,” alisema.
Pia Mwenyekiti wa kijiji cha Mikenge ulipo mgogoro huo, Lameck Mayala, amesema viongozi wa Manispaa hiyo wamechochea kwa kiasi kikubwa Kwa kupindisha ukweli juu ya barabara hiyo.