Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mindi Kasiga akieleza jambo katika Mkutano wa Mabalozi na Mwenyekiti wa Taasisi ya Zanzibar Maisha Bora (ZMBF), Mhe. Mama Mariam Mwinyi tarehe 17 Novemba, 2022. |
Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Swahiba Mndeme akichangia mada katika Mkutano wa Mabalozi na Mwenyekiti wa Taasisi ya Zanzibar Maisha Bora (ZMBF), Mhe. Mama Mariam Mwinyi tarehe 17 Novemba, 2022 |
Mke wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Taasisi ya Zanzibar Maisha Bora (ZMBF), Mhe. Mama Mariam Mwinyi akiagana na mabalozi baada ya kumaliza kikao baina yake na mabalozi hao |
Mke wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Taasisi ya Zanzibar Maisha Bora (ZMBF), Mhe. Mama Mariam Mwinyi katika picha ya pamoja na mabalozi wanawake |
Mke wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Taasisi ya Zanzibar Maisha Bora (ZMBF), Mhe. Mama Mariam Mwinyi katika picha ya pamoja na mabalozi wanawake |
Mke wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Taasisi ya Zanzibar Maisha Bora (ZMBF), Mhe. Mama Mariam Mwinyi amewahamasisha Mabalozi wanawake wa Tanzania kuiunga mkono Taasisi hiyo ili kuiwezesha kufikia malengo yake ya kuwasaidia watoto na kuwakwamua kiuchumi wanawake na vijana wa Zanzibar.
Mhe. Mama Mwinyi ametoa rai hiyo tarehe 17 Novemba, 2022 alipokutana na Mabalozi Wanawake wanaoiwakilisha Tanzania nje ya nchi katika makazi yake mjini Zanzibar.
Amesema Taasisi hiyo ambayo aliianzisha mwezi Julai 2021 imejikita katika kutekeleza malengo makuu manne ambayo ni Kuwainua Kiuchumi Wanawake wakulima wa zao la Mwani; Kuboresha upatikanaji wa Lishe bora kwa wanawake wajawazito na watoto; Kuboresha mazingira ili kuwalinda wasichana na wavulana dhidi ya vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia; na Kuiimarisha taasisi ya ZMBF ili kuiwezesha kuwa endelevu na yenye matokeo chanya kwa jamii.
Ameongeza kuwa ili kuwakwamua kiuchumi wanawake wakulima wa zao la mwani ambao ni asilimia 80 ya wakulima wote wa zao hilo, jitihada za pamoja zinahitajika ili kuliongezea thamani zao hilo ili liwanufaishe zaidi wakulima hao kuliko ilivyo hivi sasa.
Mhe. Mariam ameongeza kuwa, katika kuimarisha afya ya watoto wa kike pamoja na kukuza kiwango cha ufaulu kwa watoto hao, Taasisi hiyo imeanzisha Program ya hedhi salama kwa kutengeneza taulo za kike ambazo ni rafiki kwa mazingira.
“Taasisi yetu ina takribani mwaka mmoja tangu ianzishwe, tumejikita kuimarisha lishe kwa kina mama wajawazito na watoto na kuwasaidia wanawake wakulima wa mwani. Lakini pia tumejielekeza katika kuboresha elimu kwa watoto wa kike kwa kuwatengenezea taulo za kike ili kupunguza utoro mashuleni unaotokea wakati watoto hao wakiwa hedhi. Hivyo tunaomba mtuunge mkono nyinyi binafsi na kwa kuwashirikisha wadau mbalimbali kwenye maeneo yenu ya uwakilish ili tufikie malengo yetu” alisema Mhe. Mariam.
Kuhusu masuala ya ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto, Mhe. Mama Mwinyi amesema Taasisi yake hutoa elimu kwa wanawake ya namna ya kujilinda na kuwalinda watoto pamoja na kuwahamasisha kutoa taarifa ya matukio ya ukatili wanayofanyiwa ili sheria ichukue mkondo wake. Pia taasisi hiyo imeanzisha nyumba maalum ambayo huwasaidia wahanga wa matukio ya ukatili ambapo wakiwa hapo hujengewa uwezo kwa kupatiwa ujuzi wa fani mbalimbali ili kujikimu kimaisha pamoj ana kupatiwa msaada wa kisheria.
Kwa upande wao, Mabalozi hao walipongeza jitihada zinazofanywa na Mhe. Mama Mariam kupitia Taasisi hiyo na kueleza utayari wao wa kuisaidia ili kuiwezesha kutimiza malengo yake ambayo mengi ni miongoni mwa masuala yanayopewa kipaumbele katika majukwaa ya kikanda na kimataifa.
Mabalozi wa Tanzania wapo Zanzibar kushiriki Mkutano kati yao na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan unaofanyika kisiwani humo kuanzia tarehe 14 hadi 21 Novemba, 2022